Kwanza kabisa unapaswa kujua kwamba wateja halisi wa biashara yako wanafanya manunuzi ya kununua kwa hisia na siyo kwa fikra au mantiki.

Pia unapaswa kujua kwamba wateja wananunua kwa sababu zao binafsi na siyo kwa sababu wewe unauza.

Lakini pia unapaswa kujua, kwamba wateja watanunua kwako, kama wanavutiwa kufanya hivyo, kama kuna kitu kinawasababisha wanunue kwako na siyo kwa wengine.

Hivyo basi, ili kuwafanya wateja wako wadumu, uwe nao kwa muda mrefu, na wasikutoroke, unahitaji kutengeneza nao mahusiano bora kabisa.

SOMA; BIASHARA LEO; Huuzi Tu Biashara, Unajiuza Na Wewe Pia.

Wachukulie wateja wako kama watu na kama rafiki zako wa karibu. Chochote unachofanya hakikisha unakifanya kwa faida ya mteja na siyo kwa faida yako pekee.

Ukishajua vizuri kile unachotoa, na ukajua vizuri mahitaji ya wateja wako, kisha ukatengeneza mahusiano ya utegemezi, ambapo mteja wako anakutegemea wewe ili mambo yake yaende vizuri, hakuna anayeweza kukuibia wateja wako.

Kwa sababu wengi wanaofanya biashara, hawaelewi dhana hii ya kutengeneza mahusiano bora na wateja wao. Wao wanauza tu na hawataki mazoea, na ni kwa sababu wanakazana kumuuzia kila mtu.

Lakini wewe kazana kujenga mahusiano haya, chagua kuwahudumia wateja wanaoendana na biashara yako na siyo kila mtu, wape thamani kubwa, wajali kama watu na wataendelea kuwa na wewe kwa muda mrefu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha