“If you really want to get where you set out to go, you’re going to have to get off the wrong bus.”
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SHUKA KWENYE BASI LISILO SAHIHI…
Kama upo Dar na unataka kwenda Arusha, ukapanda basi kwa haraka, lakini njiani ukagundua basi ulilopanda haliendi Arusha bali linaenda Dodoma, njia pekee ya kufika Arusha ni kushuka kwanza kwenye basi la Dodoma.
Haijalishi unataka kiasi gani kufika Arusha, kama kwanza hutashuka kwenye basi ambalo siyo sahihi, hutaweza kufika sehemu sahihi kwako.
Kung’ang’ana kwenye basi ambalo siyo sahihi kunazidi kukupoteza na hata kukupotezea muda. Na kadiri unavyoshuka mapema, ndivyo unavyoweza kuwahi safari yako sahihi.
Kwenye maisha kuna watu wengi sana ambao wapo kwenye hali hii, wameingia kwenye njia ambayo siyo sahihi kwao, lakini hawapo tayari kuiacha njia hiyo.
Wanajikuta kwenye hali ambayo hawakuitaka, lakini hawana ujasiri wa kuondoka.
Wanaendelea kwenda tu siyo kwa sababu watafika wanakotaja, bali kwa sababu wanataka siku ziende.
Rafiki, kagua kila kitu unachojihusisha nacho na angalia kina mchango gani kwako kufikia mapengo makubwa uliyonayo.
Kama kitu hakina mchango, haijalishi umekifanya kwa muda gani au umewaahidi wengine nini, unapoteza muda na nguvu zako.
Hakikisha kwenye kila eneo la maisha yako upo kwenye basi sahihi. Una mengi ya kufanya na muda siyo rafiki kwako. Kuchagua kupoteza muda huo wa adimu kwenye maeneo ambayo siyo sahihi kwako ni kuchagua kupoteza maisha yako.
Ukishagundua basi ulilopanda siyo sahihi, shuka haraka na panda basi ambalo ni sahihi.
Hakuna muujiza wa kufika sehemu sahihi kwa kupanda basi ambalo siyo sahihi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukagua kila aina ya basi ulilopanda kwenye maisha yako na kuona kama ni sahihi kwako kufika kule unakotaka kufika.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha