Kuna watu huwa tunawaona wapo wapo tu, hawaeleweki nini wanafanya au wapi wanakwenda.

Ni rahisi kusema watu hawa hawajui wanachotaka, au ni wavivu au wazembe na kadhalika.

Lakini ukweli ni kwamba, kila mtu anajua kile anachotaka kwenye maisha yake, tena anajua kwa uhakika kwa namna anavyokitaka.

Ila tu wengi huwa hawathubutu kusema kile wanachotaka, kwa hofu kwamba wakisema basi watalazimika kufanyia kazi.

Kwa sababu kama wakisema wanataka kitu fulani, halafu hawachukui hatua, itakuwa rahisi kwa watu kuwasema kwa namna wasivyofanyia kazi kile wanachotaka.

Wakati mwingine watu wanaogopa kwamba kama wakisema wanachotaka, halafu wakakikosa, wataonekana siyo watu makini kwa wengine, wataonekana ni wakosaji, wazembe na mengine mengi.

Ninachotaka kukumbusha rafiki yangu, ni kutumia nguvu ya kutamka na kusema wazi kile unachotaka ili ikusukume kukipata.

Kukaa na malengo makubwa mwenyewe hakukupi msukumo, kwa sababu hata usipoyafikia hakuna anayekuuliza. Lakini unapoyasema malengo hayo kwa wengine, wanaanza kukufuatilia, utapata msukumo wa kufanya ili usiwaangushe watu hao.

Na siyo lazima utangaze kwa kila mtu, wala haipaswi kuwa hivyo. Chagua watu wachache ambao unawaheshimu sana, ambao hutaki kuwaangusha, na waambie kile hasa unachotaka na kwamba utakipata.

Kisha hakikisha huwaangushi watu hao kwa kukazana kukipata. Ukishawajulisha wengine ni nini hasa unataka, utalazimika kukipata, la sivyo utaonekana ni mzembe na usiye na maana.

Na kama umewaambia wengine unachotaka halafu huchukui hatua, bado pia utakuwa na kazi ya kutengeneza sababu za kuwaeleza kwa nini hufanyi au kwa nini hujapata unachotaka. Yote hayo ni kazi na hivyo utajikuta ni bora tu kufanya kuliko kutafuta sababu.

Chagua watu watakaojua nini unataka, watakaokuwa wanakufuatilia kujua umefikia wapi, ili pale unapoanza kufikiria kutokuendelea kufanya, ukumbuke namna watu hao wanavyokutegemea ufanye.

Kuweka siri kile unachotaka, hata kama unaogopa kukosolewa, unajikosesha msukumo wa kukipata, maana kilicho siri kwako, kitabaki sirini na hakitatoka kuwa uhalisia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha