Kila tunapokuwa na maamuzi ambayo tunapaswa kuyafanya kwenye maisha yetu, hatukosi sababu ya kusogeza mbele, kwa sababu maamuzi yoyote ni magumu kufanya na kwa hali ya kawaida huwa akili zetu hazipendi vitu vigumu.

Sasa kwa kusogeza kwetu maamuzi mbele, tunafika mahali na kukuta tuna maamuzi mengi ambayo tunapaswa kuyafanya na hatuna tena muda wa kusubiri. Hapa ndipo tunapokazana kufanya maamuzi mengi kwa wakati mmoja, na mengi yanakuwa maamuzi ya hovyo sana.

Unapofanya maamuzi mengi kwa wakati mmoja, unajiweka kwenye nafasi ya kufanya maamuzi mabovu.

Hii ni kwa sababu kila maamuzi unayoyafanya yana gharama kiakili, kila maamuzi unayoyafanya yanatumia nguvu kubwa sana ndani yako. Hivyo kila unapofanya maamuzi, nguvu hii hupungua. Unapofanya maamuzi mengi kwa pamoja, jinsi nguvu yako ya kiakili inavyopungua, ndivyo unavyoishia kufanya maamuzi ya hovyo.

Unajikuta unakubali au kukataa kitu ambacho kama ungekuwa na nguvu za kutosha kiakili, ungefikiri kwa kina na kuja na maamuzi tofauti.

Tunapofanya maamuzi mengi na kuchoka kiakili, kitu cha kwanza kinachopotea ni uwezo wetu wa kufikiri kwa kina na uwezo wa kufikiri kwa kina unapopotea, maamuzi yanayofuata baada ya hapo huwa ni maamuzi mabovu.

Pangilia vizuri kila maamuzi unayopaswa kufanya, kama ni maamuzi muhimu na yanayohusisha kufikiri kwa kina, fanya maamuzi hayo mapema pale unapoianza siku na fanya maamuzi machache.

Usikubali kufanya maamuzi muhimu ukiwa umeshachoka, pia epuka kufanya maamuzi mengi kwa wakati mmoja. Fanya maamuzi ukiwa na nguvu ya kutosha ya kufikiri kwa kina. Tofauti na hapo unajiandaa kufanya maamuzi mabovu ambayo yatakugharimu sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha