Daktari bingwa mmoja wa magonjwa ya akili amewahi kusema kwamba chanzo kikuu cha magonjwa ya akili kwa wengi ni kujaribu kuyakimbia majukumu yao kwenye maisha. Pale mtu anapoukataa uhalisia wa maisha yake, ndipo anapokaribisha magonjwa mbalimbali ya akili. Na hili lina ukweli mkubwa ndani yake, japo yapo magonjwa yenye sababu nyingine kama kurithi, lakini kukimbia majukumu ni kichocheo kikubwa.

Tukija kwenye maisha yetu binafsi, nimekuwa naona chanzo kikuu cha matatizo kwenye maisha ya wengi. Yaani kwa kila anayekutana na matatizo makubwa kwenye maisha yake, anayepitia changamoto mbalimbali na ambaye hafanikiwi, kuna mzizi mkuu ambao unakuwa unasababisha yote hayo.

Chanzo hicho kikuu ni mtu kukimbia uhalisia wake. Watu wengi hawapendi kujikubali kama walivyo, hawapendi kujijua wao wenyewe na kutumia kila kilicho ndani yao kuyaendesha maisha ambayo yana maana kwao. Badala yake wengi wamekuwa wanajikimbia wao wenyewe na kukimbilia kuiga maisha ya wengine. Wengi wamekuwa wanakazana kuwa kama wengine na kujisahau wao wenyewe.

Ni katika kuiga huku maisha ya wengine ndipo watu wanatengeneza matatizo mengi na ambayo yanawasumbua sana. Wengi wanajikuta wakikazana kufanya mambo ambayo hayana maana kwao ila tu waonekane nao wanafanya. Wengi wamekuwa wanakubali vitu ambavyo wangepaswa kukataa ila hawathubutu kufanya hivyo kwa sababu hawataki kuishi uhalisia wao.

Mtu mmoja amewahi kusema, watu wanatumia fedha ambazo hawana, kununua vitu ambavyo hawavihitaji, ili kuwaridhisha watu ambao hawajali.

Kama ungejua jinsi ambavyo wengi hawajali kuhusu maisha yako, ungeachana kabisa na maigizo ya maisha na kuishi yale maisha yenye uhalisia kwako, na hilo lingepunguza sana matatizo yako.

Chagua sasa kuishi maisha yako, chagua kuishi uhalisia wako, chagua kufanya yale ambayo ni muhimu na yana maana kwako na fanya kama vile hakuna anayeona, kama vile upo peke yako hapa duniani, kwa sababu kwa uhalisia, upo peke yako, ni wewe tu unayejali zaidi kuhusu wewe kuliko mtu mwingine yeyote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha