“There is no more stupefying thing than anger, nothing more bent on its own strength. If successful, none more arrogant, if foiled, none more insane—since it’s not driven back by weariness even in defeat, when fortune removes its adversary it turns its teeth on itself.”
—SENECA, ON ANGER, 3.1.5
Siku mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari HASIRA NI NISHATI MBAYA…
Wapo watu ambao wanasukumwa na hasira kufanya makubwa, na hata kufanikiwa.
Pale watu wanapokunyanyasa na ukapata hasira ya kufanya makubwa ili baadaye wakuheshimu.
Pale mtu wa karibu anapokataa kukusaidia na unapata hasira ya kufanikiwa zaidi ili aone jinsi ambavyo wewe unaweza pia.
Yote haya yanaweza kuonekana kama hasira ni nzuri na ni nishati ya kufanikiwa.
Lakini hilo ni kama utaangalia kwa upofu, ndiyo hasira inaweza kuwa nishati, lakini ni nishati mbaya.
Kwa sababu kama Seneca anavyosema, kama utafanikiwa kwa kusukumwa na hasira unaishia kuwa na kiburi, na kama utashindwa basi inakuzidishia hasira zaidi kaisi cha kukuumiza zaidi.
Na pale inapotokea kwamba yule unayempelekea hasira zako hayupo tena basi hasira hizo zinarudi ndani yako, hivyo kila hatua unayopiga unazidi kuwa na hasira ndani yako.
Tuepuke sana hasira kwenye maisha yetu, tuachane na kila hali mbaya inayoibuka ndani yetu kutoka kwa wengine na tuwasamehe kila waliotukosea, iwe ni kwa kujua au kwa kutokujua.
Ishi maisha yako kwa msukumo wa ndani yako wa kutaka kufikia uwezo mkubwa ulio ndani yako.
Usiishi maisha yako kutaka kuwaonesha na kuwakomoa wengine ambao walikusumbua kipindi cha nyuma. Hasira hazitakuwa na ukomo na zitakupoteza zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kusukumwa na uhitaji wako na siyo kwa hasira.
#HasiraNishatiMbaya, #IshiMaishaYako, #WasameheWanaokukwaza
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha