“An important place to begin in philosophy is this: a clear perception of one’s own ruling principle.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.26.15
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SEHEMU YA KUANZA FALSAFA…
Watu wengi wanaposikia falsafa basi hupata picha ya watu wanaotumia muda wao kubishana kuhusu maisha, yameanzia wapi na maana yake nini.
Wengi hufikiri ili uwe mwanafalsafa lazima usomee na kutunukiwa shahada ya falsafa.
Lakini sivyo wanafalsafa wa ustoa wanavyotuambia kuhusu falsafa.
Sehemu muhimu ya kuanzia falsafa ni kuwa na utambuzi sahihi wa msingi wa kuendesha maisha yako.
Wewe ni mwanafalsafa pale unapokuwa na msingi unaotumia kuendesha maisha yako na kuuelewa msingi huo.
Huhitaji shahada, cheti wala hata kuwaambia wengine kwamba wewe ni mwanafalsafa.
Badala yake chagua msingi wa kuyaongoza maisha yako na ishi msingi huo.
Msingi unakupa mwongozo wa yapi ya kufanya na yapi ya kutokufanya.
Msingi unakupa njia ya kujipima na kujitafakari kwa hatua unazochukua kila siku.
Msingi unakupa maana na sababu ya kuwa hapa duniani.
Usikubali kuyaendesha maisha yako bila ya kuwa na msingi unaokuongoza. Maana kama Socrates alivyowahi kusema, maisha yasiyopimwa, hayana maana kuyaishi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na utambuzi sahihi wa msingi mkuu unaoendesha maisha yako, na kuishi msingi huo kila siku.
#KuwaNaMsingi, #FalsafaNiMatendo, #YapimeNaKuyatafakariMaisha
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha