Kila mmoja wetu kuna wakati ambapo anajikuta kwenye shimo fulani katika maisha yake.
Shimo hilo ni pale unapokuwa umekwama, ulichotegemea hakiwezekani tena na hujui ni nini utafanya ili kutoka pale ulipokwama sasa.
Kila mtu anapitia hali hii, lakini wanaofanikiwa wanaishinda na kuondoka kwenye shimo wanalokuwa wameingia. Kwa upande wa pili, wale wanaoshindwa huwa hawawezi kutoka kwenye mashimo waliyoingia, wanakata tamaa na kuona haiwezekani tena. Na wengine wanaendelea kuchimba mashimo waliyopo na hivyo kuzidi kupotea.
Hakuna shimo ambalo mtu huwezi kutoka, hata liwe refu na baya kiasi gani, ukishajikuta kwenye shimo basi unaweza kutoka kwenye shimo hilo.
Na kitu pekee kitakachokutoa kwenye shimo lolote uliloingia ni hatua ambazo utachukua.
Wengi ambao wanajikuta kwenye shimo huwa wanachukua hatua za hovyo, ambazo zinazidi kuwadidimiza kwenye shimo na kuwapoteza kabisa.
Njia sahihi ya kutoka kwenye shimo ni kuchukua hatua sahihi, na hatua sahihi za kuchukua zina sifa kuu mbili;
Moja, chukua hatua ya kufanya kitu ambacho kinakujengea ujuzi mpya na wenye manufaa kwako. Hapa unajikuza zaidi wewe, na hivyo kuweza kutoa thamani kubwa zaidi ambayo itakutoa pale ambapo umekwama sasa.
Mbili, chukua hatua ya kufanya kitu ambacho kinawasaidia wengine, kitu ambacho kinaongeza thamani kwenye maisha ya wengine na kuyafanya kuwa bora zaidi ya yalivyokuwa awali. Unapotoa thamani zaidi kwa wengine, huwezi kubaki pale ulipo sasa.
Mfano wa shimo ambalo wengi wamekwama ni ajira, mtu anakuwa kwenye ajira ambayo haipendi na haimlipi, anakuwa hana maisha ya furaha. Badala ya kuchukua hatua ya kumtoa kwenye shimo hilo, anachimba zaidi shimo, wengi hukimbilia kukopa, hivyo siyo tu anakuwa na kazi asiyoipenda na isiyomlipa, bali pia anakuwa na mkopo wa kulipa, mzigo unakuwa mara mbili.
Hatua sahihi ya kuchukua pale unapokuwa upo kwenye ajira usiyoipenda na isiyokulipa ni kujifunza na kufanya biashara ya pembeni, ambayo inaongeza thamani kwa wengine. Inaweza kuwa ya bidhaa au huduma, ianze kidogo na endelea kukua kadiri unavyokwenda na hili litakutoa kwenye shimo ulilopo.
Unapojikuta kwenye shimo, hatua ya kwanza usiendelee kuchimba, kisha chukua hatua za kujiboresha wewe mwenyewe na kuongeza thamani kwa wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,