Kuna changamoto kubwa sana kwenye zama tunazoishi kwa sababu machaguo ni mengi mno.

Watu walioishi kipindi cha nyuma, hawakuwa na machaguo mengi kama tuliyonayo sasa. Kazi au biashara zilikuwa ni chache na moja kwa moja watu walielekea kwenye kile wanachofanya na kuweka nguvu zao zote hapo.

Lakini sasa hivi machaguo ni mengi, na hivyo watu hawajui wafanye nini na waache nini. Mtu anachagua kufanya kitu kimoja, labda kazi au biashara lakini anaona kazi au biashara nyingine nzuri zaidi, anashawishika kuacha ya mwanzo na kwenda kwenye hiyo nyingine. Akiwa huko anaona tena kingine kizuri zaidi, na anaendelea kubadilika kila wakati.

Mitandao ya kijamii nayo imechochea sana tatizo hili, mtu anaona mwenzake kwenye mtandao ameweka kitu alichonacho au anachofanya, ghafla na yeye anataka kuwa na kitu kama kile au kufanya kama anavyofanya huyo mwenzake.

Hapo bado kwenye kujifunza, kwa wingi wa taarifa zilizopo sasa, mtu anaweza kusoma kitabu au hata mtandaoni anakutaka na hadithi au ushuhuda wa mtu kwenye kile alichofanya akafanikiwa sana, na hapo mtu anataka kufanya alichofanya mtu huyo.

Unaweza kuona mwenyewe ni kwa nini watu wengi hawafanikiwi sasa licha ya maarifa na siri zote za mafanikio kuwa wazi. Kikwazo ni kimoja, watu wengi hawajui kwa hakika nini wanataka. Hivyo wanahangaika na kila kitu badala ya kuweka juhudi zao zote kwenye vitu vichache na kuachana na vitu vingine vyote.

Kama bado hujafanya maamuzi haya rafiki, yafanye sasa. Chagua nini unataka kufanya, chagua nani unataka kuwa, kisha weka juhudi zako zote kwenye kufanya au kupata kitu hicho. Utaona vitu vingine vizuri na vinavyovutia, lakini unapaswa kuachana navyo maana kuhangaika navyo ni kujichelewesha kufika kule unakotaka kufika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha