Kuna hadithi nyingi sana za mafanikio, kila aliyefanikiwa ana hadithi yake, na ukifuatilia hadithi nyingi, utakuta zinakinzana.
Mmoja aliyefanikiwa atakuambia alifanya hivi, mwingine atakuambia alifanya kinyume chake.
Sasa hapo unaweza kujikuta njia panda, usijue kitu gani sahihi kwako kufanya ili kufanikiwa.
Wapo pia wengi ambao wamekuwa wanabadilika kila wanaposikia hadithi za mafanikio za wengine.
Wanasikia hadithi ya mtu mmoja ambaye amefanikiwa sana kwenye kilimo cha matunda wanaanza kutafuta shamba walime matunda. Wakiwa wanatafuta wanasikia hadithi ya mwingine ambaye amefanikiwa sana kupitia biashara ya usafirishaji wanaanza kufuatilia biashara hiyo. Kabla hawajafika mbali wanasikia hadithi nyingine ya mtu aliyefanikiwa kupitia biashara ya fedha na wanaanza kufuatilia biashara hiyo.
Rafiki, haijalishi watu waliofanikiwa wamefanya nini ili kufanikiwa, wewe hutafanikiwa kwa kuiga kile walichofanya au kujaribu kuishi maisha kama yao.
Unachopaswa kujifunza kwa waliofanikiwa siyo kile walichofanya, kwa sababu huwezi kufanya kama wao.
Bali unachopaswa kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa ni misingi waliyoiishi mpaka wakafanikiwa. Misingi ndiyo itakuwezesha na wewe pia kufanikiwa kwenye chochote unachofanya, na ukabaki kuwa wewe.
Hivyo jifunze kupitia waliofanikiwa, shiriki semina na mafunzo mbalimbali, soma vitabu mbalimbali lakini mwisho wa siku kuwa wewe na usijaribu kuwa mtu mwingine yeyote. Mafunzo unayopata yanapaswa kukufanya wewe kuwa bora zaidi kwa utu wako wa tofauti na siyo kuiga wengine.
Hata wateja unaowalenga, hawatakuja kwako kama wanaona unafanana na wengine, wanakuja kwako kwa upekee ulionao, na upekee huo ndiyo unaokuwezesha kufanikiwa zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,