Hivi ni vitu vitatu ambavyo vinachangia sana kwenye biashara kufanikiwa au kushindwa.
Ukiweza kuvifanyia kazi vizuri vitu hivi vitatu kwenye biashara yako, utaweza kuikuza sana biashara yako na kufanikiwa.
Kuna hali mbili inayohusisha vitu hivyo vitatu;
Hali ya kwanza; uaminifu unakuwa juu, gharama za kuendesha biashara zinakuwa chini na huduma inapatikana haraka. Hii ndiyo hali unayopaswa kuitengeneza kwenye biashara yako, uaminifu unapaswa kuwa juu sana, baina yako na wale wanaofanya kazi kwenye biashara yako na hata kwa wateja wako pia. Kila mtu awe mwaminifu na afanye kile kilicho sahihi. Uaminifu unapokuwa juu, gharama za kuendesha biashara hiyo zinakuwa chini, kwa sababu hauhitaji sana kufuatilia kila kitu, kwa sababu uaminifu uko juu. Na pale ufuatiliaji unapokuwa mdogo, huduma zinatolewa haraka na wateja wanaridhika sana na hilo.
Hali ya pili; uaminifu unakuwa chini, gharama za kuendesha biashara zinakuwa juu na huduma haipatikani kwa haraka. Hii ni hali ambayo inaua biashara nyingi, hakuna uaminifu baina ya waliopo kwenye biashara na hata wateja hawaiamini biashara. Hivyo gharama nyingi zinatumika kuwafuatilia na kuwadhibiti watu, na kadiri ufuatiliaji na udhibiti unakuwa mkubwa, upatikanaji wa huduma unakuwa wa kuchelewa sana.
Kazana kujenga uaminifu mkubwa kwenye biashara yako na gharama za kuiendesha zitakuwa chini huku huduma ikipatikana haraka na wateja kuridhika zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,