“How much more harmful are the consequences of anger and grief than the circumstances that aroused them in us!”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 11.18.8

Ni siku mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIFANYE MAMBO KUWA MABAYA ZAIDI…
Ni tabia yetu sisi wanadamu pale mambo mabaya yanapotokea tunakazana kuyafanya kuwa mabaya zaidi.
Jambo fulani ambalo hatukubaliani nalo linatokea, hili linaibua hasira ndani yetu, na hasira hizo zinafanya mambo kuwa mabaya zaidi.

Kanuni ya mashimo inasema, ukishajikuta uko ndani ya shimo, hatua ya kwanza ni kuacha kuchimba. Halafu sasa kuangalia unatokaje kwenye shimo hilo.
Lakini wengi hawafuati kanuni hiyo rahisi kabisa, wengi wanapojikuta kwenye shimo, wanakazana kuendelea kuchimba zaidi na zaidi na hivyo kupotea zaidi.

Usiyafanye mambo kuwa mabaya zaidi, dhibiti sana hasira zako na hisia hasi ulizonazo.
Haijalishi umekutana na jambo baya kiasi gani, kuruhusu hasira zikutawale ni kufanya jambo hilo liwe baya zaidi.

Mara zote matokeo ya kile unachofanya kwa hasira huwa ni makubwa na mabaya kuliko kile kilichosababisha hasira hiyo.
Hivyo jizuie sana kuchukua hatua kwa hasira au hisia nyingine hasi pale unapokutana na mambo ambayo hukutegemea.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuzuia hasira zako ili usifanye mambo kuwa mabaya zaidi.
#HasiraHasara, #UkijikutaKwenyeShimoAchaKuchimba, #UsifanyeMamboKuwaMabayaZaidi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1