Kinachowafanya watu wengi kufikia hali ya kukata tamaa na kushindwa ni kujitenga na dunia.
Wengi hukazana na mambo yao wenyewe, na hivyo wanapokutana na ugumu au changamoto, wanaona ni wao pekee wanaopitia ugumu na changamoto hiyo.
Wanapoona wengine wakiendelea na maisha yao bila ya kuonekana kuwa na matatizo, wanapoona wengine wakionekana kuyafurahia maisha na kuweka mambo mazuri kuhusu wao kwenye mitandao ya kijamii, basi mtu anajihakikishia kwamba ni yeye pekee anayeteseka kwenye maisha.
Lakini ukweli uko wazi, hakuna ugumu au changamoto yoyote unayopitia wewe sasa hivi ambayo hakuna watu wengine wanaoipitia.
Kila unachopitia kwenye maisha yako, kuna wengine wengi ambao wanakipitia pia, lakini pia wapo ambao wana magumu na makubwa kuliko unayopitia wewe.
Hivyo jua kwamba haupo peke yako, chochote unachopitia, kuna wengine walishapitia wakashinda, na kuna wengine wengi wanapitia na kupambana nacho kwa sasa.
Kikubwa acha kujitenga na dunia, acha kujiangalia wewe mwenyewe na jichanganye na watu wengine, jifunze kwa watu wengine.
Kuwa na watu unaoshirikiana nao, ambao wanaelekea kule unakoelekea wewe. Kuwa na watu ambao unajifunza kutoka kwao, ambao wameweza kupiga hatua na kufika kule unakotaka kufika.
Na muhimu zaidi, usiyaangalie sana magumu yako, bali angalia ni kwa jinsi gani unaweza kutatua magumu ya wengine. Ukiyaangalia sana magumu yako ni rahisi kukata tamaa. Lakini unapoyaangalia magumu ya wengine, ambayo unaweza kuyatatua, unajikuta unapata jawabu la magumu yako.
Hii ni kusema kwamba, haijalishi unapitia magumu makubwa kiasi gani, kazana kuweka juhudi zako kwenye kazi au biashara yako. Kazana kutoa huduma bora kabisa kwa wale wanaokutegemea kupitia kazi au biashara unayofanya. Kadiri unavyowawezesha wengine kutatua magumu yao, ndivyo magumu yako yanavyopata suluhisho pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,