Watu wengi wamekuwa wanapoteza fursa nzuri sana pale ambapo wanakimbilia kujibu swali ambalo wameulizwa kabla hawajafikiria kwa nini swali hilo limeulizwa.

Kwenye kitabu nilichokuwa nasoma, nilikutana na kisa cha mtu aliyekuwa anauza kampuni yake, na waliotaka kununua wakamuuliza kwa nini unauza kampuni yako? Na yeye akajibu kwamba anataka kupata muda zaidi wa maisha yake na hataki kubanwa tena na biashara. Hili lilikuwa jibu la kweli kutoka ndani ya moyo wake. Waliotaka kununua wakamwambia sawa, basi tutakutafuta.

Baada ya watu hao kuondoka, muuzaji alibaki na mshauri wake, ambaye alimwambia tumeshawapoteza hao wanunuaji. Muuzaji akauliza kwa mshangao, kwa nini, mbona mazungumzo yamekwenda vizuri? Mshauri akamwambia ndiyo mazungumzo yamekwenda vizuri, lakini jibu lako la kwa nini unauza biashara siyo kitu ambacho wanunuaji wanaangalia. Wanunuaji wakigundua kwamba unauza biashara kwa sababu unataka kupumzika, wanaona kuna tatizo kwenye hiyo biashara.

Hivyo akamshauri wakati mwingine anapoulizwa swali kama hilo, ajibu anauza kwa sababu anaona biashara ina uwezo wa kukua zaidi ikimilikiwa na watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha. Na hii siyo kudanganya, kwa sababu huo ndiyo uhalisia na wanunuaji watahamasika zaidi kuinunua wanaposikia kuna ukuaji.

Nimeona hili linatufaa sana kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yetu. Pale mtu anapokuuliza swali, usikimbilie tu kujibu kile kinachotoka moyoni mwako, hata kama ni ukweli. Fikiria kwanza kwa nini mtu huyo ameuliza swali.

Kila swali ambalo mtu anauliza, kuna sababu nyuma yake na kuna majibu anayategemea. Hivyo kujua sababu hiyo na kujua mategemeo ya muulizaji, unaweza kumjibu kwa usahihi na kuweza kufikia makubaliano sahihi.

Kuna maswali mawili tu ambayo ukiulizwa unaweza kujibu bila ya kufikiri. Maswali hayo ni jina lako na namba yako ya simu. Maswali mengine yote fikiria kwanza kwa nini swali limeulizwa, tafakari kwa kina na toa majibu ambayo yanaendana na hali au mazingira uliyopo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha