“It is possible to curb your arrogance, to overcome pleasure and pain, to rise above your ambition, and to not be angry with stupid and ungrateful people—yes, even to care for them.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.8

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni jambo kubwa sana na la kushukuru kwa nafasi hii tuliyoipata leo. Siyo kila aliyelala jana amepata nafasi hii, hivyo tuitumie vizuri kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HUNA SABABU…
Pale watu wanaposhindwa kupiga hatua fulani ambayo ni muhimu kwao ili kuwa na maisha bora, huwa wanatafuta sababu ya kujipa.
Wengi husingizia mazingira waliyopo, hali iliyopo au hata kule walikotoka.
Ni rahisi kwa wengi kulaumu kwamba hawakupata misingi sahihi au hawakuandaliwa vizuri au ndivyo walivyo.

Lakini ukweli ni kwamba, hizo ni sababu tu za kuwaridhisha wale ambao hawajajitoa kweli kubadilika.
Kama unataka kubadilika kweli, ili maisha yako yawe bora saba, basi unahitaji kuondokana na sababu zote unazojipa. Kwa sababu ni za uongo na ndiyo zimekuwa zinakuzuia wewe usifanikiwe.

Asubuhi hii hebu jikumbushe hatua zote ambazo umekuwa unatamani kupiga kwenye maisha yako, kisha angalia sababu ambazo umekuwa unajipa kwa nini hujapiga hatua hizo. Anza kuhoji sababu moja moja, je ni ukweli au ni kujiridhisha tu.
Kutaka kujua kama sababu ni ukweli au kujiridhisha, angalia kama kuna wengine wameweza kufanya licha ya kuwa na vikwazo ulivyonavyo wewe.
Kama wengine wameweza kufanya, basi wewe huna sababu, ni uzembe tu.

Kama unajiambia huwezi kuingia kwenye biashara kwa sababu huna mtaji, halafu kuna wengine ambao walikuwa kwenye hali kama yako na wakaweza kuingia kwenye biashara, wewe huna sababu, unaficha tu uzembe wako.
Kama unajiambia hali ngumu ya uchumi ndiyo inakuzuia kufanikiwa, lakini katika hali hiyo hiyo wapo ambao wanapiga hatua kubwa sana, huna sababu, bali hutaki kukubali kwamba kuna uzembe unaofanya.

Pitia kila sababu ambayo umekuwa unajipa kwenye maisha yako, na angalia je hakuna walioweza kufanya licha ya kuwa na sababu hiyo? Kama wapo basi jua huna sababu, unajidanganya tu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuachana na sababu unazojipa na kuchukua hatua sahihi kuelekea kule unakotaka kufika.
#HunaSababu #KamaWengineWamewezaNaWeweUnaweza #ChukuaHatuaNaSababuZitakimbia

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1