Kujifunza ni rahisi,
Kuomba na kupokea ushauri ni rahisi,
Kuweka malengo na mipango ni rahisi,
Lakini inapofika wakati wa kuchukua hatua, hapo ndipo ugumu unapoanzia.
Kuchukua hatua ni kugumu sana kwa sababu kuna nafasi ya kushindwa, na watu wengi wamekuwa hawapendi kushindwa kwenye chochote wanachofanya.
Hivyo watu huwa wanafanya zoezi la kuahirisha kile wanachotaka kufanya mpaka pale kunapotokea nguvu kubwa inayowasukuma kuchukua hatua.
Kuna nguvu kubwa tatu ambazo huwa zinawasukuma wengi kuchukua hatua.
Nguvu ya kwanza ni msongo, hapa kunakuwa na mvutano mkali ndani yako ambao unakulazimisha uchukue hatua fulani. Bila ya kuchukua hatua msongo huu hautulii kabisa. Mfano upo njia panda kati ya kufanya kitu A na kitu B, na una muda mfupi wa kufanya maamuzi, utalazimika kuchukua hatua hata kama hujawa tayari.
Nguvu ya pili ni tamaa, hapa unakuwa na kitu unachotamani sana kukipata, kitu ambacho usipochukua hatua utakikosa. Hapa unasukumwa kuchukua hatua ili upate kile ambacho unakipenda sana.
Nguvu ya tatu ni hofu, hapa unakuwa na kitu unachohofia na kama hutachukua hatua basi mambo yatazidi kuwa mabaya. Hivyo unalazimika kuchukua hatua ili kuvuka hofu hiyo.
Rafiki, zipo njia mbili za kutumia nguvu hizi tatu;
Njia ya kwanza ni kuzitumia nguvu hizo kwako wewe binafsi, pale unapopanga kuchukua hatua fulani, ziweke nguvu hizo ili zikusukume kuchukua hatua. Jiweke kwenye hali ambayo itakulazimisha kuchukua hatua. Mfano ahidi kuwa umekamilisha kazi ndani ya muda mfupi kuliko unavyopaswa na ikitokea umeshindwa kufanya hivyo basi usilipwe. Hapa unakuwa umeibua nguvu zote tatu.
Njia ya pili ni kutumia nguvu hizi kwa wengine, pale ambapo unataka wengine wachukue hatua fulani, watengenezee nguvu hizo tatu, waweke kwenye msongo, jua na gusa tamaa zao na ibua hofu itakayowasukuma kuchukua hatua.
Tumia nguvu hizi tatu kwa nia njema na siyo kutaka kujinufaisha wewe zaidi ya wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,