“Here’s a lesson to test your mind’s mettle: take part of a week in which you have only the most meager and cheap food, dress scantly in shabby clothes, and ask yourself if this is really the worst that you feared. It is when times are good that you should gird yourself for tougher times ahead, for when Fortune is kind the soul can build defenses against her ravages. So it is that soldiers practice maneuvers in peacetime, erecting bunkers with no enemies in sight and exhausting themselves under no attack so that when it comes they won’t grow tired.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 18.5–6
Kuiona siku hii mpya ya leo ni jambo la kushukuru sana.
Siyo kwa akili zetu wala ujanja wetu,
Bali ni kwa bahati tu.
Tumeiona siku hii kwa sababu kazi yetu hapa duniani bado haijakamilika.
Hivyo tutumie vizuri nafasi hii ya leo kufanya yale muhimu zaidi kwetu.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAANDALIZI NI WAKATI MAMBO NI MAZURI…
Wanajeshi huwa wanafanya mazoezi magumu na mazito wakati wa amani, ili vita inapokuja, wawe tayari kwa mapambano.
Na kadiri mwanajeshi anavyotokwa jasho jingi wakati wa mazoezi na maandalizi, ndivyo atakavyotokwa damu kidogo wakati wa mapambano.
Kila mmoja wetu anapaswa kujiandaa kwa nyakati ngumu na mbaya wakati ambapo mambo ni mazuri.
Maana huo ndiyo wakati ambao watu hujisahau sana na pale wanapokutana na magumu wakiwa hawana maandalizi, wanasumbuka sana.
Chagua siku ambazo utajipa mazoezi ya kukosa kile ambacho umezoea kuwa nacho.
Chagua siku ambazo utakula chakula cha hali ya chini kabisa, hata kama una uwezo wa kula chakula chochote utakacho.
Chagua siku ambazo utavaa mavazi ya hadhi ya chini kabisa hata kama una uwezo wa kuvaa mavazi ya hadhi yoyoye utakayo.
Chagua siku ambazo utachagua kulala chini bila ya godoro wala shuka, hata kama una kitanda kizuri na mashuka mazuri.
Hayo ni mazoezi madogo madogo ambayo yatakufanya kuwa imara na kukuandaa kukabiliana na chochote kinachoweza kutokea mbele yako.
Kwa kufanya mazoezi haya, siyo tu utakuwa umejiandaa, bali pia utakuwa umeishinda hofu.
Kwa sababu kitu kinachowasumbua wengi kwenye kupoteza walichonacho ni ile hofu wanayokuwa wamejijengea.
Kwamba nitakosa chakula kizuri cha kula au mavazi mazuri ya kuvaa au malazi mazuri.
Lakini unapojiweka kwenye hali hizo kabla hata hujazifikia, unajiuliza, kwani hiki ndiyo nilikuwa nahofia? Mbona ni cha kawaida kabisa?
Kuwa na maandalizi bora wakati mambo ni mazuri, ili mambp yanapokuwa mabaya uwe imara na usitetereke.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujiwekea maandalizi ya mabaya unayoweza kukutana nayo kwenye maisha yako. Chagua baadhi ya vitu utakavyojinyima leo ili kujiimarisha kabla hujakutana na uhaba halisi.
#MaandaliziNiKablaYaVita #JinyimeUlichozoea #IshindeHofuKwaKufanyaUnachohofia
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1