“A stupid person should keep silent. But if he knew this, he would not be a stupid person.” —MUSLIH-UD-DIN SAADI

Mpumbavu anapaswa kukaa kimya,
Lakini kama angelijua hilo, asingekuwa mpumbavu.
Njia pekee ambayo watu wanaweza kujua ujinga wako ni kupitia yale unayoongea.
Hakuna njia nyingine,
Na kila mtu yuko tayari kuongea kila kitu na kuanika upumbavu wake.

Upo usemi kwamba mpumbavu akikaa kimya anaweza kudhaniwa ni mtu mwenye busara.
Kuwa bahili wa maneno yako, ongea pale ambapo ni muhimu pekee, na kama siyo muhimu kaa kimya.
Siyo lazima uwe na maoni kwenye kila jambo,
Siyo lazima na wewe uwe na mchango wako.
Maneno unayotoa hovyo hovyo yanakugharimu sana.

Hii pia inahusisha yale unayoandika mitandaoni,
Chunga sana vidole vyako, vinakupoteza na kuanika ujinga wako.
Usikimbilie kuweka kila kitu mitandaoni,
Usikimbilie kujibu na kubishana mitandaoni,
Usijipe kazi ya upolisi wa mitandaoni, kuamua nani kaweka kitu kizuri na nani kaweka kitu kibaya.
Kama mtu kaweka kitu mtandaoni ambacho hukubaliani nacho achana nacho, kipuuze, usianze mabishano mtandaoni.

Tunasahau sana burasa ndogo ndogo kama hizi na baadaye tunakuja kujuta baada ya kusema au kuandika kitu.
Wewe jizuie sana kwenye kusema na kuandika hovyo, utapunguza changamoto nyingi.

Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kukaa kimya pale unapokuwa huna jambo muhimu la kusema au kuandika.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania