Wakati unaweka mipango yako mikubwa ya fedha, kuna watu watakukatisha tamaa, wengine watakubeza.
Watakuambia ya nini ujisumbue na utajiri, wakati fedha hainunui furaha, huku wakikuonesha matajiri ambao hawana furaha au hawafurahii maisha yao.

Sasa iko hivi rafiki, iwe unaambiwa na wengine au unajiambia mwenyewe kwamba utajiri hauleti furaha, kwa nini uamini maneno matupu?
Si ujaribu mwenyewe?
Fanya hivi, panga kuwa tajiri mkubwa, jua kiasi cha fedha unachotaka na kisha weka juhudi kupambana kufikia kiasi hicho.
Halafu kama utakipata na usiwe na furaha, gawa utajiri huo kwa wengine.

Utajiri siyo kilema kwamba ukishakipata utadumu nacho milele.
Pambana uupate, halafu kama siyo mzuri kama ulivyofikiri, ugawe kwa wengine, utakuwa wa msaada zaidi kuliko kuendelea kujifariji kwamba utajiri siyo mzuri.

Usikubali kuambiwa au kujiambia kwa maneno matupu, jaribu ujionee mwenyewe.
Na anapotokea yeyote kukukatisha tamaa, kukuambia utajiri hauleti furaha, mwambie akupe mfano wake mwenyewe, wa jinsi alipata utajiri halafu haukumpa furaha.
Kama hana mfano wake yeye mwenyewe, bali anatumia mifano ya wengine mpuuze na endelea na mpango wako.

Uwe na usiku mwema, usiku wa kuamua kuwa tajiri na kuwapuuza wote wanaobeza fedha na itajiri.
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania