Ni rahisi kuwapa watu ushauri pale wanapokuwa na matatizo au changamoto fulani. Lakini sisi wenyewe tunapokuwa kwenye tatizo au changamoto hiyo hiyo, hatuwezi kutumia ushauri wetu wenyewe.

Hii ni kwa sababu huwa tunajiaminisha kwamba tatizo tulilonalo sisi ni tofauti na matatizo wanayokuwa nayo watu wengine. Lakini huo siyo ukweli, ni kujidanganya na kujifariji.

Iko hivi rafiki, tatizo lolote unalopitia sasa, siyo jipya kabisa wala la tofauti. Huenda ndiyo mara ya kwanza kwako kupata tatizo la aina hiyo, lakini wapo watu wengine wengi tu walishalipata huko nyuma au wanalipitia sasa na wengine wengi watakuja kulipitia siku zijazo.

Hivyo hatua ya kwanza kabisa unapokuwa kwenye tatizo au changamoto yoyote ni kujiuliza nani amewahi kuwa na tatizo kama hilo na aliwezaje kulitatua.

Na hapa ndipo inapokuja njia bora kwako kupata suluhisho la tatizo lolote unalopitia, kwa sababu watu hao waliotatua matatizo yao, wameandika vitabu au kutoa mafunzo mbalimbali kuhusiana na tatizo hilo ambayo ukiyapata yatakusaidia.

Pia jiulize ni watu gani wanaopitia tatizo hilo kwa sasa, ambao wanakazana kulitatua, hawa unaweza kushirikiana nao na kwa pamoja mkatatua na kupiga hatua.

Na mwisho, ukishatatua tatizo au changamoto yako, jua kuna wengine watakuja kukumbana nalo siku zijazo. Hivyo andika kitabu au weka kwenye mfumo ambao wengine wanaweza kujifunza kupitia uzoefu wako.

Unapoanza na mtazamo huu kwamba tatizo lako halina tofauti, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulitatua na hata kuwanufaisha wengine kupitia utatuzi wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha