2312; Ukishafanya Maamuzi…
Kinachofuata ni kuyatekeleza, kujifanyia tathmini na kuboresha kadiri unavyokwenda.
Na siyo kuanza kuyahukumu maamuzi yako mwenyewe baada ya kuwa umeyafanya, hata kama umekosea kwenye kuyafanya, kujihukumu haitasaidia. Bali unapaswa kujitathmini na kuyaboresha.
Pia siyo kupoteza muda kutaka kila mtu aelewe na kukubaliana na maamuzi hayo. Wengi hawataelewa na hata watakaoelewa hawatakubaliana nayo. Ila utakapozalisha matokeo ya aina fulani, wataona manufaa yake.
Na muhimu zaidi, siyo kusubiri mpaka uone uko tayari ndiyo utekeleze maamuzi uliyofanya, anza mara moja kutekeleza, maana maamuzi hayana maana yoyote kama hakuna utekelezaji.
Kufanya maamuzi ni hatua moja, yale yanayofuata baada ya kuwa umefanya maamuzi yanachangia sana matokeo yatakayotengenezwa na maamuzi hayo.
Fanya maamuzi na chukua hatua, kama ulikosea, jifanyie tathmini na boresha kadiri unavyochukua hatua na kupata matokeo.
Kocha.