2370; Nje Na Ndani…
Kwa kila unachofanya, kuna namna mbili za kukiangalia. Kukiangalia kwa nje na kukiangalia kwa ndani.
Unakiangalia kitu kwa ndani pale unapofuatilia kila kinachofanyika kwa undani kwenye kitu hicho.
Hapo unajali mambo madogo madogo yanayokijenga kitu hicho.
Unakiangalia kitu kwa nje pale unapoangalia picha kubwa unayotaka kufikia kwenye kitu hicho na kuangalia inafikiwaje. Hapo unajali mambo makubwa ya kukisukuma zaidi kile unachofanya.
Unahitaji kuwa na mlinganyo sahihi wa pande hizi mbili kwenye kile unachofanya, zote uzipe nafasi na kuzifanyia kazi ili unachofanya kifanikiwe.
Wengi hawana mlinganyo huo, huwa wanaegemea zaidi eneo moja.
Wanaoegemea zaidi kuangalia ndani, wanajikuta wakifanya kitu vizuri, lakini hawapigi hatua kubwa. Hivyo wanabaki wamedumaa pale pale. Hapa msingi unakuwa imara, ila hakuna kikubwa kinachojengwa.
Wanaoegemea zaidi kuangalia nje, wanaweza kujenga kitu kikubwa, lakini kisichokuwa na misingi sahihi, hivyo kinaanguka haraka na vibaya. Hatua zinazopigwa ni kubwa, lakini hazina tija, maana anguko linakuwa katibu.
Unapokuwa na mlinganyo sahihi, unajenga msingi sahihi kwa kuweka msisitizo wa ndani na kujenga kitu kikubwa kwenye msingi huo kwa kuweka msisitizo wa nje.
Chukua mfano wa biashara.
Anayefanya biashara kwa kuangalia ndani zaidi anaiendesha biashara yake vizuri, anajua kila kinachoendelea kwenye biashara na kufuatilia kwa karibu kila kitu.
Hilo linamchosha na anajikuta hakuna makubwa anayofanya, biashara iko vile vile miaka na miaka.
Anayeifanya biashara kwa kuangalia kwa nje zaidi anakuwa na mawazo makubwa ya kuikuza, anachukua hatua kubwa za mabadiliko. Lakini hafuatilii kwa karibu yanayoendelea kwa ndani. Anapambana kuikuza zaidi biashara lakini kinachotokea ni anguko kubwa kwa kuwa mambo ya msingi kabisa hayazingatiwi.
Kufanikiwa kwenye biashara, lazima uwe na mfumo mzuri unaosimamia yale yote ya msingi na ambao unaufuatilia mara kwa mara. Na pia lazima uwe na ndoto kubwa unazoendelea kuziangalia na kujisukuma kuzifikia.
Haya mawili yatahitaji muda wako mwingi, na yule anayeweza kuweka muda wa kutosha kwenye yote mawili ndiye anayefanikiwa sana.
Kocha.