2385; Kula na Kumeng’enya…

Unapokula chakula, hakiingii moja kwa moja kwenye mwili wako kama ulivyokila.
Badala yake kinameng’enywa kwanza, kinavunjwa kwenye vipande vidogo vidogo na kisha kufyonzwa kwenye mwili.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kusoma. Kusoma ni kama kula, unachosoma siyo kinachoingia kwenye akili yako, bali kile unachochakata.

Hivyo usifurahie tu kusoma, bali pia pata muda wa kuchakata yale uliyojifunza, kuona jinsi unavyoweza kuyatumia kwenye maisha yako na kuchukua hatua.

Unakula chakula kingi, lakini kinachofyonzwa ni kidogo. Kadhalika kwenye usomaji, unasoma vitu vingi lakini utakavyoweza kutumia moja kwa moja ni vichache.

Pia unaweza kula ukavimbiwa, ukatapika au kuharisha. Hayo pia hutokea kwenye usomaji, hasa pale unapoingiza maarifa yasiyo sahihi.

Tenga muda wa kusoma, lakini pia pata muda wa kutafakari yale uliyosoma na jinsi unavyoweza kuyatumia moja kwa moja kwenye maisha yako.

Kocha.