#SheriaYaLeo (7/365); Pesa Na Mafanikio.

Kwa walio wengi, hitaji la kupata pesa na mafanikio linaweza kuwa motisha mkubwa kwao kuwasukuma kufanya makubwa.
Kwa watu wa aina hii huona hakuna haja ya kuhangaika kulijua kusudi la maisha yao. Huona huko ni kupoteza muda na hivyo huachana na hilo na kuhangaika na kupata pesa na mafanikio.

Watu hao wanakamia sana kupata pesa na mafanikio, lakini mwisho wake kinachotokea ni tofauti. Kile wanachotaka sana kukipata hawakipati.
Tunajua hili kwenye maisha, kwamba pale unapotaka kupata sana kitu ndiyo unakikosa.
Pale unapolazimisha kitu kiende kwa namna fulani ndiyo kinakwenda kwa namna tofauti kabisa.

Mfano pale unapojilazimisha ulale, ndiyo usingizi unapotea kabisa.
Pale unapolazimisha uwe na furaha ndiyo unaipoteza kabisa.
Pale unapotaka sana watu wakuelewe na kukukubali ndiyo hawakuelewi kabisa.

Mambo yote mazuri kwenye maisha yetu huwa yanakuja pale ambapo tumetingwa na mambo mengine kabisa.
Ni pale unapofikiria vitu vingine ndiyo usingizi unakupitia.
Ni pale unapochagua kuwa wewe ndiyo wengine wanakuelewa na kukukubali.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye pesa na mafanikio.
Unapokamia sana kuvipata, ndiyo unazidi kuvisukuma kwenda mbali na wewe.
Unapotaka sana kupata pesa na mafanikio, ndivyo unavyozidi kuvikosa.

Badala yake pesa na mafanikio huja pale mtu unapokuwa unahangaika na vitu vingine tofauti kabisa.
Ni pale unapokuwa umeweka umakini wako wote kutoa thamani kubwa, kufanya kile kilicho bora ndiyo unashangaa pesa na mafanikio makubwa vinakuja kwako.

Hata ukiwaangalia wale waliofanikiwa sana, msukumo wao mkubwa siyo pesa na mafanikio. Hayo huwa ni matokeo tu ya wao kuweka umakini wao mkubwa kwenye mambo mengine.
Wanakuwa na msukumo mkubwa ndani yao ambao hauhusiani na pesa wala mafanikio, bali unahusiana na kusudi na ndoto kubwa walizonazo.
Kwa msukumo wa aina hiyo, pesa na mafanikio huwa ni matokeo wanayokutana nayo.

Sheria ya leo; Weka umakini wako wote kwenye kulijua na kuliishi kusudi la maisha yako na pesa na mafanikio vitakuja kwako kama matokeo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma