2514; Uasi usio na msingi wowote.
Tunajua umuhimu wa kukataa mazoea na kuepuka kundi ili kuweza kufanikiwa.
Kwamba tunajua ni vigumu sana kufanikiwa kwa kufanya mambo ambayo yamezoeleka kufanyika na yanafanywa na kila mtu.
Lakini pia haimaanishi unapaswa kutembea kwa mikono kwa sababu kila mtu anatembea kwa miguu.
Kuna baadhi ya mazoea unapaswa kuendelea nayo kwa sababu huna mbadala bora zaidi.
Kwa maneno mengine usikatae mazoea au kuepuka kundi kwa sababu tu unataka uonekane wewe siyo kama wengine.
Huo ni uasi usio na msingi wowote, hauna tofauti ni kijana aliye kwenye balehe (adolescent) ambaye anataka tu kupingana na wazazi wake kwa sababu anaona na yeye ni mtu mzima.
Kataa mazoea na epuka kundi pale ambapo una mbadala bora zaidi. Pale ambapo una kitu cha kufanya ambacho kinahitaji namna ya tofauti ili kifanikiwe.
Na lazima ujue kabisa kwamba kufanya hivyo kuna gharama yake kubwa, kuanzia kuvuka mazoea yako mwenyewe mpaka kuvuka vikwazo vya wengine.
Ndiyo maana hupaswi kupoteza nguvu zako kupingana na watu kwenye mambo yasiyo na manufaa kwako.
Kubaliana nao na nenda nao hata kama mambo yanaonekana hayana maana kabisa.
Kama kupingana nayo hakuna msaada kwenye mafanikio yako, achana na hilo.
Lakini inapokuja kwenye mambo yanayoathiri mafanikio yako, hapo kataa kabisa mazoea ya aina yoyote ile yanayokwenda kuzuia usipate mafanikio unayotaka.
Hatua ya kuchukua;
Kupinga na kubishana na watu ni kitu kinachochukua muda wako, nguvu zako na umakini wako. Kuanzia sasa, usipinge wala kubishana na yeyote kwenye mambo yasiyohusiana na mafanikio yako. Kubaliana na watu hata kama wanakosea, ili upunguze kupoteza rasilimali zako muhimu.
Tafakari;
Ukikutana na mtu anayekuambia kwa imani yake 3 + 3 = 5 na ameshikilia hilo kweli kweli, kubaliana naye na endelea na yako.
Ukimfanyia mtu kazi, ambapo mlipatana saa moja ni elfu 30 na umefanya masaa 2 na yeye anataka kukulipa elfu 50 kwa sababu kwa imani yake 30 + 30 = 50, kataa hilo na vunja hayo mazoea ili ulipwe kilicho sahihi kwako.
Kocha.