2532; Ngumu Ndiyo Sahihi.
Kwa zama tulizopo sasa, mambo tunayokabiliana nayo ni mengi kiasi kwamba kufanya maamuzi ni zoezi gumu kidogo.
Kuna taarifa nyingi za kupitia katika kufanya maamuzi yako.
Lakini muda wa kuzipitia zote ndiyo huna.
Kuvuka hilo, unahitaji kujijengea njia za mkato za kufikia maamuzi kwa haraka.
Japo njia hizo hazitakuwa na ufanisi wa asilimia 100, zitaokoa muda wako mwingi ambao utaweza kuutumia kwenye maeneo yenye tija zaidi.
Moja ya njia za mkato katika kufanya maamuzi ni kuangalia ugumu au urahisi wa kitu.
Kama kitu ni kigumu kufanya, kinakuwa sahihi zaidi kuliko kile ambacho ni rahisi kufanya.
Kile ambacho ndani yako unapata ugumu kukifanya, maana yake kinakusukuma kutoka nje ya mazoea yako.
Kile ambacho wengi wanakwepa kukifanya maana yake kinahitaji juhudi kubwa, wakati wengi ni wavivu.
Kwa kufanya maamuzi kwa kigezo hiki cha ugumu unajiweka kwenye nafasi kubwa ya kufanya maamuzi sahihi na yenye tija zaidi kwako.
Hatua ya kuchukua;
Ni vitu gani umekuwa unakwepa kufanya kwa sababu ni vigumu kwako?
Ni vitu gani ambavyo sehemu kubwa ya jamii inakwepa kuvifanya?
Hivyo ndivyo vitu vyenye thamani zaidi kama utakuwa tayari kuvifanya.
Chagua kilicho kigumu na kitakuwa sahihi kuliko kilicho rahisi.
Tafakari;
Kundi kubwa la watu huwa halipo tayari kufanya mambo magumu, ila huwa linakimbilia nambo rahisi. Ukiona kitu kinaeleweka na kukubalika na watu wengi, siyo kitu sahihi sana au kama ni sahihi basi hakiwezi kuwa na manufaa makubwa kwako.
Kocha.