#SheriaYaLeo (36/366); Kusanya Ujuzi Mwingi.
Lengo lako kuu kwenye mafunzo unayoyapata ni kujifunza na kukusanya ujuzi mwenye kwenye yale maeneo yanayokuvutia na kukuhamasisha.
Kama baadaye mambo yatabadilika na kulazimika kubadili kazi au biashara unayofanya, ujuzi mwingi uliojijengea unakupa fursa ya kufanya hivyo.
Lakini pia utakuwa tayari unajua jinsi ya kujifunza na kujijengea ujuzi wa aina tofauti.
Kwa zama za mabadiliko makubwa tunazoishi, kuwa na ujuzi mwingi na kuweza kujifunza ujuzi mpya kwa haraka ndiyo silaha pekee ya kukuwezesha kuvuka changamoto mbalimbali ambazo lazima utakutana nazo.
Kipindi cha nyuma, ubobezi ilikuwa kitu kigumu kwa sababu ujuzi ulikuwa umefichwa na wachache waliochaguliwa ndiyo walioweza kuupata.
Lakini kwa sasa kila aina ya ujuzi unaoweza kuwa unautaka unapatikana kwa urahisi kabisa.
Mtandao wa intaneti umerahisisha sana kujifunza na kujijengea ujuzi wa aina mbalimbali.
Unachohitaji ni kujua ujuzi unaotaka kujijengea kisha kujua maeneo sahihi ya kujifunza ujuzi huo. Kuna mitandao mbalimbali ya kujifunza na pia vyuo vingi vinatoa mafunzo yao kwa njia ya mtandao.
Na muhimu zaidi, kupitia mtandao unaweza kukutana na waliobobea ambao utajifunza chini yao.
Sheria Ya Leo; Kujijengea ujuzi mwingi ndiyo ufunguo wa kuvuka nyakati za mabadiliko makubwa tunazoishi. Kuweza kuunganisha pamoja ujuzi huo uliojijengea ndiyo njia ya kufika kwenye ubobezi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu