2646; Watu hawabadiliki, wanakufa.
Kwenye moja ya mahijiano aliyokuwa anafanyiwa, bilionea Elon Musk aliulizwa kwamba anafanya uwekezaji mkubwa sana kwenye teknolojia na anga, mbona hawekezi kwenye kuongeza umri wa watu kuishi?
Elon alitoa jibu ambalo lilinifanya nifikiri kwa kina kuhusu asili yetu kama binadamu na namna bora ya kuendana na hilo.
Elon alijibu haoni kama kuongeza umri wa watu kuishi itakuwa na manufaa kwa jamii na dunia kwa ujumla.
Kwa sababu kadiri watu wanavyoishi kwa muda mrefu ndivyo jamii itakavyodumaa.
Anaeleza kwamba mawazo yale yale yataendelea kuwepo kwenye jamii kwa muda mrefu, kwa sababu watu hawafi.
Akasisitiza zaidi kwamba watu huwa hawabadiliki, ila huwa wanakufa.
Hiyo ina maana kwamba watu wakishakuwa na mawazo au mrengo wa aina fulani, huwa hawabadiliki kirahisi.
Wataendelea kusimamia hayo maisha yao yote.
Hivyo kama watu hawafi, mawazo fulani yatatawala sana na mapya yatakosa nafasi.
Hivyo kufa kwa watu japo kunaumiza, lakini ndiyo kunafanya jamii ipige hatua.
Nilitafakari jibu hilo kwa kina na kuona kwa uhalisia kwamba ni kweli.
Angalia hata serikali inapotaka kufanya mabadiliko kwenye eneo fulani.
Wanaokuwa wakipinga sana ni wale waliopo kwenye eneo hilo kwa muda mrefu.
Na serikali inapoona upinzani ni mkubwa, huwa inajipa muda, inasubiri mpaka wale waliokuwepo kufa na baadaye mabadiliko yanakuja kuwa rahisi.
Kadhalika kwenye uongozi wa kila ngazi, kuanzia chini mpaka juu kabisa. Mabadiliko ni vigumu sana kufanyika na watu wale wale waliopo.
Ni mpaka watu hao watoke, kwa muda wao kuisha au kwa kifo ndiyo mabadiliko makubwa huwezekana.
Hatua ya kuchukua;
Kama kuna watu wanakusumbua kwenye kubadilika, jua hawatabadilika, hata kama wanakuahidi hivyo.
Cha kufanya ni kuwaondoa kwenye nafasi walizopo kama hilo lipo ndani ya uwezo wako.
Kama lipo nje ya uwezo basi subiri mpaka watakapokufa.
Huwaombei wafe na wala huharakishi vifo vyao, ila unasubirisha mambo yako mpaka hapo watakapoondoka.
Tafakari;
Hatua kubwa tulizopiga kama jamii ya binadamu ni kwa sababu mawazo ya zamani yanakufa na kutoa nafasi kwa mawazo mapya.
Mawazo ya zamani yasipokufa, kwa wale wanaoyashikilia kufa, mawazo mapya hayawezi kupata nafasi na jamii inadumaa.
Kocha.