#SheriaYaLeo (150/366); Usichukulie chochote kwa ubinafsi.
Katika safari ya maisha utakutana na watu mbalimbali, ambao watafanya mambo ambayo hukutegemea wafanye.
Ni rahisi kuchukulia hayo kibinafsi, kuona wamefanya ili kukuonea na mtazamo mwingine wa aina hiyo.
Lakini hilo siyo sahihi, watu hawafanyi lolote kwa ajili yako, bali wanafanya kwa ajili yao binafsi.
Watu wanafanya vitu kwa maslahi yao na siyo kwa kukuwinda, kukukomoa au kukuonea.
Chukulia yote hayo kama mchezo.
Kama upo ulingoni na unapigana ngumi, bondia unayepambana naye anapokupiga ngumi siyo kwa sababu anakuchukia au ana visa na wewe.
Bali ni kwa sababu anataka ushindi.
Kadhalika wale wanaotaka kukutapeli au wanaokutumia kupata nafasi fulani siyo kwa sababu wanakuchukia, bali wapo kwenye mchezo wa kutaka kile wanachotaka wao.
Ukiyachukulia maisha hivi kama mchezo, utaweza kuona wazi nia za watu kwenye yale wanayofanya.
Usiruhusu hisia zako zikutawale na uone wanafanya kukuonea.
Ona ni sehemu ya mchezo na wewe tumia mbinu za mchezo kukabiliana na hilo.
Sheria ya leo; Chukulia maisha na kila kinachoendelea kama mchezo. Chochote watu wanafanya usichukulie binafsi, bali jua ni sehemu ya mchezo. Jua wanafanya kwa maslahi yao binafsi na siyo kuhusu wewe. Kwa kujua hilo utaweza kukabiliana na hayo vizuri.
#NidhamuUafilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji