2686; Maelezo ni yale yale.

Kila unapopanda ndege, maelezo ya usalama ni yale yale.
Wahudumu wanarudia kutoa maelezo ya usalama ya hatua za kuchukua inapotokea dharura.

Hata kama kila mtu kwenye ndege tayari anajua maelezo hayo, bado ataendelea kuyatoa.

Hata kama hakuna anayesikiliza wakati anatoa maelezo hayo, bado ataendelea kuyatoa.

Wajibu wake siyo kuangalia matokeo au wapokeaji, bali wajibu wake ni kukamilisha mchakato.

Hivyo kabla ya ndege kuruka ni wajibu wa mhudumu kutoa maelezo ya usalama kwa abiria wote.
Na hilo hufanyika kwa msimamo mara zote.

Kuna funzo kubwa sana hapa kuhusu safari ya mafanikio, umuhimu wa kukaa kwenye mchakato.
Huo ndiyo wajibu wetu mkuu wa kupambana nao.

Hatupaswi kuhangaika na matokeo wala kuangalia wengine wanapokea na kuchukuliaje.
Tunachopaswa kuhangaika nacho ni nini sisi tunafanya.
Maana tukikamilisha kufanya tunachopaswa kufanya, kwa msimamo bila kuacha, kwa hakika tutafanya makubwa sana.

Wengi hatufanyi hivyo kwa sababu ya uvivu na uzembe. Tunachoka haraka kurudia mambo yale yale kila wakati.
Tunapoona matokeo yanachelewa tunaacha na kwenda kuhangaika na mengine.

Na hayo ndiyo yanapelekea wengi kuwa wamehangaika na vitu vingi, ila wanakuwa hawapati matokeo mazuri na makubwa.
Kaa kwenye mchakato, tekeleza wajibu wako na endelea kufanya hivyo kwa msimamo bila kuacha.

Hatua ya kuchukua;
Jiulize ni vitu gani unafanya kama mchakato kila siku kwenye maisha yako bila kujali matokeo au watu wanakuchukuliaje.
Kama tayari unavyo vitu hivyo endelea.
Kama huna tengeneza sasa vitu hivyo ili uweze kukomaa navyo wakati wote bila kuacha.

Tafakari;
Ingekuwa kufanya kitu mara moja kunatosha, kila mtu angekuwa amefanikiwa. Maana kufanya mara moja ni rahisi.
Mafanikio yanakutaka ufanye vitu mara nyingi na kwa kujirudia rudia bila ya kuchoka.
Uendelee kufanya hata kama unaowalenga hawajali au matokeo huyaoni kwa haraka.
Kilicho muhimu ni kukaa kwenye mchakato.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining