Ni usemi ambao kila mtu anaujua, lakini kama tunavyojua, kujua na kufanya ni vitu viwili tofauti kabisa.
Tunajua mengi, lakini hatuyafanyii kazi na hivyo hatunufaiki na yale tunayojua.
Wakati mwingine tunasahau kama tunayojua tunapaswa kuyatumia.
Tukirudi kwenye kinga ni bora kuliko tiba, kuzuia matatizo ni rahisi kuliko kuyatatua yakishatokea.
Huwa tunakwepa gharama kidogo ya kuzuia tatizo, baadaye tunakuja kulipa gharama kubwa ya kulitatua tatizo.
Lakini pia mazoea yamekuwa kikwazo kufanyia kazi yale tunayojua, kwa kuwa tumezoea kufanya namna fulani, hatuoni umuhimu wa kufanya tofauti.
Hadithi kubwa kwenye manufaa ya kinga inahusisha kada ya afya. Ambapo kipindi cha nyuma, vifo vya wakinamama wanaojifungua vilikuwa vikubwa mno.
Daktari mmoja aliyeitwa Ignaz Semmelweis, mwaka 1847 alipendekeza njia ya kupunguza vifo hivyo, ambayo hata haina gharama kubwa. Njia hiyo ilikuwa ni kwa wahudumu wa afya kunawa mikono kabla ya kumzalisha mama mjamzito.
Mazoea ya zamani yalikuwa ni wahudumu wa afya kuwazalisha wamama bila kunawa mikono, na hivyo kusambaza vimelea vya magonjwa kwa wamama hao. Lakini kwa kuwa mazoea ni magumu kuvunja, Ignaz alipingwa na kukataliwa na mpaka anakufa, madaktari wenzake hawakukubaliana na pendekezo lake.
Ni miaka mingi baadaye ilikuja kujulikana alikuwa sahihi na unawaji wa mikono unazuia mno kupunguza usambazaji wa magonjwa.
Kadhalika kwa chanjo mbalimbali, chukua mfano wa ugonjwa wa polio, ugonjwa uliokuwa hatari kiasi kwamba mtu alipoupata alikufa na kama hakufa basi alibaki na ulemavu wa kudumu.
Lakini ikagundulika chanjo ambayo imeutokomeza kabisa ugonjwa huo duniani. Hii ni mifano miwili, lakini ipo mingi mno kwenye kila eneo la maisha.
Lakini bado watu ni wabishi, wanapenda kuishi kwa mazoea kuliko kuishi kwa namna ambayo inawapunguzia matatizo na changamoto.
Jiulize kwenye kila eneo la maisha yako, ni mazoea gani unayoyaishi na kinga ipi ukiifanyia kazi utapunguza matatizo unayokuwa nayo.
Labda ni kipato hakitoshelezi, madeni makubwa, mahusiano yenye migogoro na mengine, lazima kuna kinga ambayo ukiifanyia kazi, itazuia matatizo hayo kujirudia rudia na kuwa kikwazo kwako.
Kila wakati jikumbushe kinga ni bora kuliko tiba, hivyo unapojikuta kwenye tatizo au changamoto yoyote, jiulize ungewezaje kuikinga isitokee kisha kuanzia hapo uwe ndiyo utaratibu wa maisha yako.
Matatizo yanayowasumbua wengi ni machache, ila yanayojirudia rudia, ukiishi msingi huu wa kinga, utapunguza mengi mno.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
asante kocha
LikeLike
Karibu
LikeLike
Ahsante.
LikeLike
Karibu
LikeLike
Kweli kocha, kinga ni bora kuliko tiba.
LikeLike
Hakika
LikeLike