2688; Kipi unachokumbuka?
Unapokuwa unahangaika na mambo yanayopita, kama habari na mitandao ya kijamii, unaweza kuona kama ni muhimu sana na usipofanya hivyo utapitwa na mengi.
Lakini huko ni kujidanganya,
Ni kukubali akili yako ikuhadae kwa uvivu ambao akili yako unao.
Inajaribu kuepuka mambo magumu na muhimu na kuhangaika na mambo rahisi na yasiyo muhimu.
Jiulize swali hili, chagua siku moja kwenye miezi mitatu iliyopita na jiulize kipi unachokumbuka kwenye habari na mitandao uliyokuwa unafuatilia?
Ni sifuri, hakuna kikubwa unachoweza kuwa unakumbuka kwenye yale unayohangaika nayo.
Siku hiyo uliyochagua huenda uliona ni mambo ya muhimu sana.
Lakini leo muda umepita na wala hukumbuki tena.
Kuna funzo kubwa sana hapa, kwamba tunahangaika na mambo mengi ambayo hayana tija yoyote.
Yanapokuwa mbele yetu yanaonekana muhimu, lakini baada ya muda tunakuwa tumeyasahau kabisa.
Kwa kujifunza hili tunapaswa kubadili namna tunatumia muda wetu.
Tunapaswa kuacha kuhangaika na mambo yanayosahaulika.
Badala yake tuhangaike na mambo yanayoweza kuacha alama ya kudumu kwetu.
Kusoma vitabu vizuri ni kitu kinachoacha alama, hata kama hutakumbuka kitabu kizima, lakini kuna namna kitabadili kabisa mtazamo wako.
Kujenga kitu chenye thamani kwa wengine, iwe ni biashara, huduma, ujuzi n.k, ni kitu kinachoacha alama inayokumbukwa kwa muda mrefu.
Kukuza mtandao wako na kuboresha mahusiano na watu wengine ni kitu ambacho kitadumu kwa muda mrefu na kuwa na manufaa makubwa.
Rafiki, muda ni wako na wewe ndiye mwamuzi wa mwisho.
Amua kama utaendelea kuupoteza kwenye mambo ambayo utayasahau haraka sana. Au utautumia kwenye vitu ambavyo matokeo yake yanadumu kwa muda mrefu.
Hatua ya kuchukua;
Pitia matumizi yako ya muda kwa wiki moja iliyopita. Orodhesha kila ulichofanya kwenye kila muda wako kwa wiki moja iliyopita.
Kisha pitia kimoja kimoja na jiulize kipi kinaacha alama inayodumu kwa muda mrefu.
Vyote ambavyo haviachi alama acha kuvifanya.
Tengeneza orodha ya vitu ambavyo hutakuwa unavifanya tena.
Na hapo vitu kama kufuatilia habari, kuzurura kwenye mitandao ya kijamii na mengine kama hayo yanapaswa kuwa kwenye orodha hiyo na uachane nayo kabisa.
Tafakari;
Tatizo la muda ni huwa huoni wakati unaupoteza, ni baadaye kabisa ndiyo unakuja kugundua mengi uliyokuwa unahangaika nayo yamekupotezea muda.
Kuzuia hilo, orodhesha yale ambayo yana historia ya kukupotezea muda kisha yapige marufuku kwenye maisha yako.
Utaokoa muda mwingi ambao utaweza kuutumia kufanya makubwa.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining