2696; Ukilinganisha na nini?

Utawasikia watu wakisema, maisha ni magumu.
Na hapo unaweza kujiuliza ukilinganisha na nini?

Je maisha ni magumu ukilinganisha na kifo?
Au maisha ni magumu ukilinganisha na maumivu makali mtu unayopata ukiwa unaumwa?

Kama upo hai na huna maradhi yanayokuumiza kila wakati, maisha siyo magumu kama unavyojiambia.

Utawasikia pia watu wakisema biashara ni ngumu.
Ambapo utajiuliza wanasema ngumu wakilinganisha na nini?

Je biashara ni ngumu ukilinganisha na kutokuwa na biashara kabisa?
Au biashara ni ngumu ukilinganisha na ajira ambayo ina ukomo wa kipato na haina uhuru wa muda?

Kama una biashara, siyo ngumu kama unavyojiambia, bali ndivyo ilivyo.

Rafiki, kwenye maisha mambo kutokuwa rahisi kama unavyotaka wewe haimaanishi kwamba ni magumu.
Bali ndivyo yalivyo.
Na ukitaka kudhibitisha hilo, kwa chochote unachosema ni kigumu, linganisha na mbadala wake.
Na hapo utaona hicho unachosema ni kigumu ndiyo afadhali.

Kwa chochote unachotaka kwenye maisha yako ni lazima ujitoa sana, kwa viwango vya juu ndiyo ukipate.
Usidanganyike na njia zozote za mkato za kupata kile unachotaka.

Na kama kuna kitu unaona ni rahisi kuliko ulichochagua, ni kwa sababu hujakifanya.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapojikuta unasema mambo ni magumu, jaribu kulinganisha na mbadala wake.
Na hapo utagundua wazi kwamba mambo siyo magumu kama unavyochukulia.
Japo yanahitaji uweze kujitoa kweli kweli.

Tafakari;
Kwa kuwa mambo siyo rahisi haimaanishi kwamba ndiyo magumu kabisa.
Kwa chochote unachoona ni kigumu, mbadala wake ni mgumu zaidi.
Hivyo badala ya kuhangaika kutafuta urahisi, komaa na kile ulichochagua mpaka upate matokeo mazuri.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining