2749; Kama inabidi ulazimishwe, kuna tatizo.
Siku za karibuni nilikuwa naangalia mahojiano ya aliyekuwa mchezaji bora kabisa wa mpira wa kikapu Kobe Brayant.
Aliulizwa yeye kama kiongozi alikuwa anawasukumaje wachezaji wenzake ili waweze kufanya vizuri kama timu.
Jibu ambalo Kobe alitoa lilinifikirisha sana na nikaona siyo tu kwenye michezo, bali ni kwenye kila eneo la maisha.
Kobe alisema; “Kama inabidi nimlazimishe mchezaji kwenda kwenye mazoezi, hapo kuna tatizo. Na sina namna ya kumsaidia mtu wa aina hiyo. Napenda mtu ambaye tayari ana msukumo na mapenzi makubwa ndani yake kwenye mchezo huu. Yule asiye na mapenzi kwenye mchezo sina la kufanya naye, sitaki hata kuongea naye.”
Ni maneno mafupi lakini yaliyobeba ujumbe mkubwa mno.
Ni kweli kabisa kwamba kama inabidi ulazimishwe kufanya kitu ndiyo utakifanya, hakuna namna utafanikiwa kwenye kitu hicho.
Na ushahidi upo wazi kabisa.
Angalia watu wengi wanaofanya kazi za kuajiriwa, wanaweza kuwa kwenye kazi hizo kwa miaka mingi ila hakuna hatua wanapiga.
Na hiyo ni kwa sababu wanakuwa hawazipendi kweli kazi hizo.
Wanachokuwa wanataka ni mshahara tu.
Hawafanyi chochote bila kulazimishwa au kutishiwa.
Ndiyo maana huwa wanawahi kazini pale kunapokuwa na njia ya kupima uchelewaji.
Wanatafuta kila namna ya kukwepa kazi. Wanaweza hata kwenda hospitali kudanganya wanaumwa ili tu wapewe siku za mapumziko.
Wanaofurahia sana ijumaa na kuichukia Jumatatu.
Rafiki, nakuandikia haya kwa sababu kubwa moja, usipeleke huo mtazamo kwenye biashara na safari yako nzima ya mafanikio.
Kama kitu unachofanya hakikupi msukumo wa ndani.
Kama hakikufanyi uwe tayari kuanza na kuchelewa kumaliza.
Kama hakikukoseshi muda wa kuhangaika na mambo mengine.
Na kama inabidi watu wengine wakulazimishe na kukushurutisha ndiyo ufanye.
Basi jua kuna tatizo mahali.
Na kwa hakika, hakuna namna utafanikiwa.
Safari ya mafanikio tayari yenyewe tu ni ngumu, kabla hujaweka kingine chochote.
Sasa pata picha unaweka na uzito wako, kwa kutaka usukumwe kwenye hiyo safari.
Usijidanganye na wala usikubali kudanganywa.
Kama hakuna moto mkubwa unaowaka ndani yako na kukuzuia usitulie, hakuna namna unaweza kutoboa kwenye hii safari ya mafanikio.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye safari yako ya mafanikio, je unao msukumo wa kufanya kutoka ndani yako au ni mpaka usukumwe na wengine?
Kama ni mpaka usukumwe na kulazimishwa na wengine, basi jua kuna tatizo kubwa mahali na mafanikio utaishia kuyatamani tu, ila siyo kuyafikia.
Tafakari;
Kama unachofanya hakina msukumo mkubwa ndani yako, usipoteze nacho muda wako.
Achana nacho na nenda kwenye kile ambacho una msukumo mkubwa wa ndani.
Safari ya mafanikio tayari ni ngumu, usiongeze zaidi ugumu wake kwa kufanya ambayo huna msukumo nayo mkubwa wa ndani.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed