2750; Siyo pale unapojisikia.

Huwezi kufanikiwa kama unafanya vitu pale unapojisikia kufanya.
Mafanikio yanataka nidhamu kubwa sana ya kupanga na kufanya iwe unajisikia au la.

Na hiyo ndiyo tofauti kuu kati ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wote wanakuwa na ndoto kubwa.
Na wote wanaweka mipango ya kufikia ndoto hizo.

Ila tofauti inaonekana kwenye ufanyaji.
Wanaoshindwa wanafanya pale wanapojisikia kufanya.
Na kwa sababu kujisikia hutokea mara chache, wanashindwa kufanya kwa viwango ambavyo vitawapa mafanikio.

Wanaofanikiwa wanafanya mara zote, iwe wanajisikia kufanya au la. Wao swala la kujisikia au kutokujisikia halina nafasi. Wanapanga na kufanya, bila ya kujali nini kinaendelea.

Na hivyo ndivyo ilivyo kwenye maeneo yote ya maisha yetu.
Unaweza kula pale unapojisikia, lakini haitakuchukua muda mrefu kabla njaa haijakuadhibu vya kutosha kama hutakula kwa kiwango sahihi.
Unaweza kuoga pale unapojisikia, lakini usipooga muda mrefu mwili wako unaathirika.

Usifurahie tu kupanga, je unatekeleza kama ulivyopanga bila ya kujali nini kinaendelea?
Kwa sababu kama unaweza kuruhusu chochote kile kiingilie mipango yako, basi ni kiashiria kwamba huwezi kufanikiwa.

Mafanikio yanahitaji nidhamu na kujitoa kwa hali ya juu sana.
Ingekuwa rahisi, kila mtu angekuwa amefanikiwa.
Siyo rahisi, lakini inawezekana.
Hivyo na wewe unaweza pia.

Hatua ya kuchukua;
Rejea mipango yako ya mafanikio, je umekuwa unatekeleza kama ulivyopanga? Au kuna vitu umekuwa unaruhusu vivuruge mipango yako? Anza sasa kusimamia mipango yako bila ya kuruhusu chochote kuvuruga. Jenga nidhamu ya hali ya juu kabisa kwenye kutekeleza kama ulivyopanga na utaweza kufanya makubwa sana.

Tafakari;
Mafanikio hayana siri, miujiza wala njia za mkato. Njia kuu ya mafanikio ipo wazi kwa watu wote. Na wengi wanaianza njia hiyo. Ila wanaofanikiwa ni wachache ambao wanakaa kwenye njia hiyo bila kutoroka. Wengi wanashindwa kwa sababu hawakai kwenye njia kwa muda mrefu mpaka wapate matokeo mazuri.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed