2751; Kujua, kuweza na kufanya.

Kama leo hii, utaacha kabisa kujifunza vitu vipya, yaani usijifunze chochote kipya, ila ukafanyia kazi yale ambayo tayari unayajua, bado utapata mafanikio makubwa sana.

Kwa mfano ukaweka juhudi kubwa kwenye kazi/biashara yako kila mara.
Ukawa na matumizi madogo kuliko kipato chako na hivyo kuweka akiba na kuwekeza.
Ukala kwa afya, kufanya mazoezi na kupumzika.
Na ukatenga muda kwa ajili ya wale muhimu kwako.
Ukifanya hayo kwa msimamo kwa kipindi kirefu, lazima utapata mafanikio makubwa.

Hakuna asiyejua hayo.
Na wala hakuna asiyeyaweza.
Bali wengi hawayafanyi.
Na hata wanapofanya, huwa siyo kwa msimamo.

Wengi hawafanikiwi.
Siyo kwa sababu hawajui,
Au hawawezi.
Bali kwa sababu, hawafanyi.

Hivyo kama bado hujapata mafanikio unayoyataka, mahali pa kuanza kuangalia siyo hujui nini, tayari unajua vya kutosha.
Wala huhitaji kuangalia sana uwezo wako, tayari unao wa kutosha.
Mahali la kuanza kuangalia ni kwenye kile unachofanya.
Kwa nafasi kubwa hufanyi, au hata kama unafanya basi ni kwa uvivu na uzembe, kwa namna ambayo haina tija.

Hapo ndipo umuhimu wa kuwa na kocha unapokuja.
Kwa sababu kocha hakufundishi tu au kukuonyesha uwezo mkubwa ulionao.
Bali pia anakusimamia kuhakikisha unafanya.

Unafikiri wachezaji bora kabisa hawajui jinsi ya kucheza mchezo wao? Tayari wanajua sana.
Je unadhani wachezaji hao hawana uwezo mkubwa kwenye michezo yao? Wanao sana.
Lakini wachezaji wote bora kabisa wanakuwa na makocha.
Kwa sababu kujua na kuweza pekee haviwatoshi kuwa bora.
Wanahitaji kusimamiwa ili wafanye kwa tija na uhakika.

Hatua ya kuchukua;
Leo jitafakari, kama bado hujafika unakotaka kufika, kikwazo siyo ujuzi wala uwezo, kikwazo kikubwa ni kufanya.
Kuna kitu hufanyi au hata kama unafanya siyo kwa viwango vya kuridhisha.
Leo jikumbushe yale ya msingi kabisa kufanya kwenye kila eneo la maisha yako ili uweze kufika kule unakotaka kufika.
Kisha fanya yote kwa msimamo wa hali ya juu sana.

Tafakari;
Kama unasoma hapa, una bahati kubwa kwenye maisha yako, tayari unaye kocha wa kukusimamia ili ufanye.
Swali ni je unamtumiaje kocha huyo ili kuhakikisha unafanya kwa msimamo na viwango vya hali ya juu kabisa?
Jua kitu pekee kinachokukwamisha ni kwenye ufanyaji.
Hivyo mtumie kocha wako vizuri ili uweze kufanya makubwa na kwa msimamo wa hali ya juu.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed