2752; Niseme vibaya kwenye mengine yote, lakini siyo kwenye hiki kimoja.
Kama binadamu, najua sijakamilika.
Nina maeneo ambayo nina uimara mkubwa.
Na maeneo ambayo nina udhaifu mkubwa.
Najua kuna watu wananisema vibaya kwenye mambo mbalimbali, mengine ya kweli na mengine siyo ya kweli.
Wapo wanaoweza kuwa wanasema sijali, nina roho mbaya, napenda sana fedha, sina muda na wengine na kadhalika.
Na kulingana na mtazamo wao kwenye maisha, wanaweza kuwa sahihi.
Kitu kimoja kizuri kwenye maisha na ambacho kinanisaidia ni kutokujali sana wengine wananichukuliaje.
Jinsi wengine wanavyonichukulia siyo biashara yangu, bali ni biashara zao wenyewe.
Kilicho muhimu kwangu ni kufanya kile kilocho sahihi ili kuweza kufikia ndoto kubwa nilizonazo.
Ambapo pia kilocho sahihi kwangu kinaweza kisiwe sahihi kwa wengine.
Ndiyo maana sijali sana vile ambavyo wengine wananichukulia.
Nimewaruhusu watu waniseme vibaya kwa mambo mengine yote kwenye maisha.
Lakini kuna kitu kimoja ambacho sitakubali mtu yeyote aniseme nacho vibaya.
Kitu hicho ni ufanyaji kazi.
Sitakubali mtu yeyote aniite mvivu.
Nitahakikisha hata kama watu wataniita mambo mabaya yote, lakini watakiri kitu kimoja, kwamba kweli mimi ni mchapa kazi.
Na sitafanya hivyo kwa maneno bali vitendo.
Nitaweka kazi kwa vitendo kiasi kwamba hata kama mtu ananichukia na kunidharau kiasi gani, ataheshimu ufanyaji kazi wangu.
Kazi ndiyo eneo pekee ambalo nina udhibiti nalo kwenye maisha.
Kazi ndiyo eneo pekee ambalo hakuna anayeweza kuwa na tafsiri yake binafsi.
Hivyo nimechagua eneo la kazi kama sehemu ya kila mtu kuniheshimu.
Kila siku nitaweka juhudi kubwa kwenye kazi kiasi cha kila mtu kukubali kwamba ninachapa kazi.
Kamwe sitaruhusu mtu yeyote apate sababu ya kuniita mzembe na mvivu.
Hata kama mtu hanikubali kwa kila kitu, basi angalau atakubali ufanyaji wangu kazi wa juhudi kubwa.
Japo najua wapo watakaokuwa na maoni kwamba kufanya kazi sana siyo kuzuri.
Lakini hakuna anayeweza kuyapinga matokeo ya kazi.
Hatua ya kuchukua;
Ni kwa namna gani upo tayari kuitumia kazi kujitofautisha na watu wengine wote?
Upo tayari kiasi gani kuweka kazi kiasi cha kuwanyima watu sababu ya kukuita mzembe na mvivu?
Tafakari;
Juhudi unazoweka kwenye kazi ni kitu ambacho kipo ndani ya udhibiti wako kwa asilimia 100.
Tumia juhudi zako za kazi kama kitu cha kukutofautisha na wengine na kukujengea heshima kubwa kwa kila mtu.
Waruhusu watu wakuseme vibaya kwa mengine yote, lakini siyo kwenye kazi.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed