2786; Hujashindwa, ni uvivu tu.

Rafiki, kama kuna kitu chochote unachojiambia umeshindwa, siyo kweli.

Kama bado upo hai, hakuna chochote unachokuwa umeshindwa.
Bali unakuwa tu na uvivu wa kuendelea.

Kila hadithi ya watu waliofanikiwa ina somo moja kubwa, kufanya kitu mara nyingi na kwa muda mrefu bila kupata matokeo mazuri.
Wamerudia rudia sana ndiyo wakaweza kufanikiwa.

Tumejifunza sana kuhusu Thomas Edison aliyejaribu zaidi ya mara elfu 10 ndiyo akafanikiwa kuvumbua taa ya umeme.
Kuhusu Michael Jordan aliyekosa zaidi ya mara elfu 9 kufunga kwenye mpira wa kikapu.
Abraham Lincoln aliyeanguka kwenye chaguzi nyingi.
Nelson Mandela aliyekaa gerezani miaka 27.

Hao ni wachache tu, lakini hadithi ya kila aliyefanikiwa, kwa maneno mengine ambaye tunamjua sana leo licha ya kutokuwepo kwake, ina hali hiyo.
Kuendelea kufanya kwa kurudia rudia na kwa muda mrefu licha ya kutokupata matokeo aliyotarajia.

Sasa turudi kwako, ni kipi unasema umeshindwa?
Je umeshakifanya zaidi ya mara elfu 10 kama Thomas Edison?

Umeanzisha biashara moja ikafa, au hata kama ni tatu, halafu unataka kuitangazia dunia kwamba umeshindwa kwenye biashara?

Unaongea na wateja mara moja, au hata mbili na tatu na wanakataa kununua, halafu unataka kuitangazia dunia kwamba umeshindwa kuuza?

Umeshindwana na mtu mmoja, au hata wachache, kwenye mahusiano, halafu unataka dunia ijue kwamba umeshindwa kwenye mahusiano!

Rafiki, leo nakueleza ukweli kama ulivyo.
Wewe hujashindwa, ni uvivu tu unakusumbua.
Kama hujapata chochote unachotaka, siyo kwa sababu huwezi kukipata, bali kwa sababu una uvivu wa kuendelea kuweka juhudi bila kuchoka.

Kama kitu unakikubali au kukitaka kweli, utaendelea kukifanya bila ya kuacha haijalishi ni matokeo gani unayapata.
Kama kukutana na kikwazo mara moja unakimbia, hujakitaka kitu kweli na hivyo uvivu unakuzidi nguvu.

Hatua ya kuchukua;
Huenda ulishafanya, lakini leo rudia tena. Amua kwa hakika nini unataka kwenye maisha yako na jiambie wazi hakuna kushindwa. Kama tu upo hai, utaendelea kupambania kile unachotaka. Hakuna chochote kitakachokuwa kikwazo kwako usiendelee kufanya.
Kataa kila aina ya uvivu na kuwa mfanyaji. Hiyo ndiyo njia ya uhakika ya kupata chochote unachotaka.

Tafakari;
Ukirisha matope mengi kwenye ukuta, kuna ambayo yatanasa, japo mengi yataanguka.
Ushindi unatokana na wingi wa wewe kufanya.
Ukifanya mara chache na kuacha unakuwa umechagua kushindwa.
Ukifanya mara nyingi bila ya kuacha unajiwekea uhakika wa kushinda.
Hivyo kama unataka ushindi wa uhakika, fanya bila kuacha. Usijali ni matokeo gani unayoyapata, wewe fanya.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed