#SheriaYaLeo (290/366); Pima watu kama wana wivu.

Wivu ni moja ya hisia ambazo binadamu huwa tunakuwa nazo.
Ni hisia inayochochewa na hali ya mtu kujilinganisha na wengine na kutokupenda pale wengine wanapokuwa wamemzidi.
Wivu huweza kumsukuma mtu kufanya mabaya na kuwadhuru wengine kwa kutokupendezwa na namna walivyowazidi.

Katika mahusiano na kushirikiana kwako na wengine, ni muhimu kuwapima kama wana wivu ili ujue jinsi ya kwenda nao kwa tahadhari.

Unachopaswa kufanya ni kumweleza mtu habari zako njema, labda kupandishwa cheo, biashara kukua au mengine mazuri, kisha kuangalia nyuso zao jinsi wanapokea taarifa hizo.
Watajifanya kukupongeza, lakini nyuso zao na sauti zao zitabeba hali ya msongo na kutokufurahishwa na mambo hayo mazuri kwako.

Kadhalika unaweza kuwaeleza watu kuhusu mambo mabaya ambayo umekutana nayo kwenye maisha yako, labda kufukuzwa kazi, kupata hasara au kupoteza vitu muhimu.
Watajifanya kukupa pole, lakini sura na sauti zao zitaonyesha wamefurahishwa na hilo.

Watu wenye wivu wanaweza kujifanya wako pamoja na wewe, lakini sura na sauti zao huwa zinadhihirisha wazi kwamba hawapo na wewe.
Ni muhimu kuwapima wale wanaokuzunguka ili ujue wapi sahihi kuwashirikisha mambo yako.

Sheria ya leo; Unapaswa kuweka umakini wako kwenye sura na maneno ya watu, vimebeba ujumbe mzito kuliko kile anachosema. Ni vyema kuwajua mapema watu wenye wivu ili kujihadhari nao wasije wakakudhuru.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji