2787; Jipe uhakika mwenyewe.
Kitu kimoja kinachotukwamisha sana kwenye maisha ni kukosa uhakika.
Hilo ndiyo limekuwa linatuzuia kufanya maamuzi na hata tukifanya maamuzi tunashindwa kuyasimamia.
Kwa mfano nikikupa wateja 10 ambao kwa uhakika watanunua kwako, ila wanachosubiri ni wewe uwatembelee, utafanya kila namna kuwatembelea. Hutakuwa na sababu yoyote ya kukuzuia, kwa sababu unao uhakika.
Lakini inapokuja kwamba inabidi utembelee wateja 100 ndiyo upate 10 ambao watanunua, unaanza kupata kila aina ya sababu kwa nini huwezi kufanya hivyo.
Kukosa uhakika kutafanya uwe na sababu lukuki za kushindwa kufanya.
Huo ni mfano mmoja, lakini ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha yako.
Ukiona kuna jambo muhimu unalopaswa kufanya lakini hulifanyi, jua sababu kuu ni kukosa uhakika.
Hivyo basi, unaweza kuvuka hilo kwa kuanza na kujipa uhakika wewe mwenyewe.
Kwa chochote unachotaka na kufanya, jipe uhakika kwamba kitakuwa.
Ndiyo, jipe uhakika kabisa kwamba kitakwenda vile ulivyopanga.
Uhakika huo ndiyo utakaokuwezesha wewe ufanye bila ya kuacha.
Na jibu ni ndiyo, pamoja na kujipa uhakika na kufanya, bado hutapata matokeo uliyotegemea.
Je utazuiaje hilo lisikukatishe tamaa na kukuzuia kufanya?
Kuna njia moja ya kufanya hilo, sahau kuhusu matokeo yaliyopita na jiwekee uhakika kwenye kile unachokwenda kufanya.
Yaani yaliyopita yanakuwa yamepita, uhakika wako unaweka kwenye kile unachopaswa kufanya, kilicho mbele yako na siyo kilichopita.
Rafiki, sikudanganyi, hili ni gumu na ndiyo maana wengi hawafanyi.
Na kama ilivyo kwenye mengi yanayohusu mafanikio, siyo rahisi na ndiyo maana wengi huwa hawayafanyi.
Yaani inabidi uwe kama vile umechanganyikiwa, uukatae uhalisia na kutengeneza uhalisia wako mwenyewe, ambao haupo kabisa.
Kama alivyowahi kunukuliwa mwanafalsafa mmoja akisema; watu wa kawaida huwa wanaenda na uhalisia wa dunia, watu wasio wa kawaida huwa wanaifanya dunia iendane na uhalisia wao. Hivyo maendeleo ya dunia yanatokana na watu wasio wa kawaida.
Hivi unadhani waliogundua ndege waliendana na uhalisia wa dunia?
Kila aina ya ugunduzi mpya ambao umewahi kufanyika hapa duniani, ulitokana na watu kwenda kinyume na uhalisia uliokuwepo.
Na waliweza hilo kwa sababu walijipa uhakika kwamba kuna matokeo tofauti na yaliyozoeleka.
Na ndiyo, watu waliwacheka na kuwaoja wamechanganyikiwa.
Lakini mwisho wa siku wao ndiyo walikuwa na kicheko kikubwa.
Hatua ya kuchukua leo;
Ni uhakika gani unaojipa ambao unakwenda kinyume na uhalisia uliozoeleka kiasi cha watu kukucheka na kukuona kama umechanganyikiwa?
Kama jibu ni hakuna, unajizuia mwenyewe kufanikiwa.
Tangu ukiwa mtoto kuna ndoto za tofauti umekuwa nazo, ambazo uliwahi kuwaeleza wengine wakakuambia achana nazo, hazifai au haziwezekani. Ukawasikiliza na kuzika ndoto hizo.
Kosa kubwa sana ambalo umewahi kufanya kwenye maisha yako.
Fufua ndoto zote kubwa ambazo umewahi kuwa nazo, jipe uhakika kwamba zinawezekana na zipambanie.
Tafakari;
Akili yako ya ndani (subconscious mind) ambayo ndiyo ina nguvu kwenye maamuzi unayofanya, huwa haijui ukweli au uongo. Yenyewe hupokea kila wazo ambalo unaipa na kulifanyia kazi.
Hivyo unapojipa uhakika na kuamini hivyo, haijalishi kama ni uongo au ukweli, akili hiyo hufanyia kazi uhakika huo.
Ni kupitia kuamini na kukaa kwenye uhakika wako ndiyo unaweza kufanya makubwa.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed