2789; Thamani ya sekunde moja.

Taa za barabarani za siku hizi ni tofauti na za zamani.

Zamani taa zilikuwa zinawaka tu, kijani, njano, nyekundu.

Lakini siku hizi taa hizo zinakuwa na muda pia, muda ambao unaanzia juu na kupungua mpaka unapoisha.

Kwa mfano kama taa inawaka kwa dakika moja, basi inaanza kwa sekunde 60 ambazo zinaenda zikipungua mpaka 0 ambapo taa inazima.

Kupitia taa hizi nimekuwa nashangazwa sana na jinsi watu wanavyoithamini sekunde moja.

Kama taa ya kijani ndiyo inawaka na imebali sekunde moja izime, watu wanakimbiza magari zaidi kuwahi sekunde hiyo moja.

Na kama ni taa nyekundu inawaka, ikiwa imebali sekunde moja izime, watu wanaanza kuendesha magari kuwahi.

Wakati mwingine huwa najikuta nikicheka sana na jinsi watu wanakimbizana na sekunde moja barabarani.

Lingekuwa jambo zuri sana kama watu wangekuwa wanathamini sekunde moja hivi kwenye kila eneo la maisha.

Lakini watu watanangaika na muda njiani, ila wakishafika huko wanakokimbilia wanaenda kupoteza muda.

Hebu angalia rahisi, unakimbilia kuokoa sekunde moja kwenye taa barabarani, halafu unaenda kupoteza saa nzima ukizurura mitandaoni au kufanya mambo yasiyo na tija.

Kama kweli unathamini muda, dhihiridha hilo kwenye maeneo yote ya maisha yako.

Kadhalika kwenye fedha, nguvu na umakini wako.
Unaweza kukazana kuomba upunguziwe elfu moja kwenye kitu cha maana unachonunua, halafu ukaishia kupoteza fedha zaidi ya hiyo kwenye mambo yasiyo na tija.

Au inapokuja kwenye kusoma kitabu unafanya haraka kwa sababu unaona huna muda. Lakini ukiingia mitandaoni unatumia muda mwingi bila ya kuharakisha.

Huwa ninaamini, bila ya shaka yoyote kwamba rasilimali tulizonazo zinatutosha kufanya makubwa yote tunayotaka kufanya.
Tunapokwama ni kwenye kuzitumia rasilimali hizo vizuri.

Anza sasa kutumia rasilimali ulizonazo vizuri na kwa tija na utaweza kufanya makubwa utakavyo.

Hatua ya kuchukua;
Jitathmini wewe mwenyewe kuona ni maeneo gani madogo madogo ambayo umekuwa ukikazana kutumia rasilimali zako vizuri, halafu unakuja kupoteza rasilimali hizo hizo kwenye maeneo makubwa?
Kila mmoja wetu kuna namna anafanya hili, tukiweza kupeleka umuhimu huo tunaoweka kwenye mambo madogo na kuweka kwenye makubwa, hakuna kitakachotushinda kufanya.

Tafakari;
Wazungu huwa wana kauli inasema; ‘penny wise, pound foolish’. Yaani kujali sana vitu vidogo na kupuuza makubwa. Ni maeneo gani ya maisha yako umekuwa unajali sana mambo madogo madogo na kupuuza yaliyo makubwa? Anzia hapo na utaweza kufanya makubwa zaidi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed