2791; Uwanja wa nyumbani.

Kwenye michezo yote, huwa kuna dhana ya uwanja wa nyumbani.
Kwamba timu inakuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda inapokuwa inacheza kwenye uwanja wa nyumbani.

Hivyo timu inapokuwa inacheza uwanja wa ugenini, huko hucheza kwa kujilinda zaidi ili isifungwe. Timu ikiwa ugenini haiangalii sana kusinda, bali inakazana kujizuia isifungwe.

Nguvu za ushindi wa timu zinakuja kutumika kwenye uwanja wa nyumbani.
Hapo ndipo timu inashambulia hasa kuhakikisha inapata ushindi mkubwa.

Kwenye uwanja wa nyumbani timu ina nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu ina mashabiki wengi, ni mazingira ambayo imezoea na ina udhibiti wa vitu vingi kuliko ikiwa ugenini.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio.
Kuna uwanja wa nyumbani na uwanja wa ugenini.

Inapokuja kwenye mafanikio, uwanja wa nyumbani ni pale unapofanya kitu kinachotoka ndani yako kweli, kitu unachopenda kufanya hata kama hakuna anayekulipa.

Hapo ni uwanja wa nyumbani kwako kwa sababu unakuwa na msukumo mkubwa wa kukifanya kitu ambacho kina uhakika wa kukupa ushindi mkubwa.

Uwanja wa ugenini kwenye safari ya mafanikio ni pale unapofanya vitu ambavyo hupendi kufanya au havitoki ndani yako kweli.
Unapofanya vitu kwa sababu tu unataka kupata fedha.
Unaviona vikiwa kazi ngumu kwako, ambapo ni mpaka usukumwe au kutishiwa ndiyo unafanya.

Kama mpo wafanyabiashara wawili eneo moja na mnauza kitu kinachofanana, kwa bei sawa na mnalenga soko moja.
Unafikiri nani ana nafasi kubwa ya kuuza zaidi?
Anayeipenda kweli biashara hiyo na anafanya kutoka ndani yake?
Au ambaye haipendi na anaifanya ili tu apate hela ya kula?
Jibu unalo.
Sasa ligeuze kwako.

Hatua ya kuchukua;
Leo jiulize na kujijibu, kwenye safari ya mafanikio uliyopo, je unacheza uwanja wa nyumbani au wa ugenini?
Kama upo uwanja wa nyumbani kazi yako ni moja tu, kushambulia kwa ajili ya kupata ushindi mkubwa.
Kama upo uwanja wa ugenini, kuna mawili ya kufanya, kwenda uwanja wa nyumani au kugeuza uwanja huo wa ugenini kuwa wa nyumbani.
Lolote kati ya hayo mawili unaweza kufanya na ukajiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindi.

Tafakari;
Muda, nguvu na umakini ni rasilimali muhimu kwenye safari ya mafanikio ambazo zina uhaba mkubwa.
Rasilimali hizo unapaswa kuzipeleka moja kwa moja kwenye mashambulizi na siyo kujilinda.
Ndiyo maana kucheza uwanja wa nyumbani kuna fursa kubwa ya kufanikiwa kuliko uwanja wa ugenini.
Ujue uwanja wako wa nyumbani na utawale huo. Adui au mshindani yeyote anayekuja kukukabili kwenye uwanja wako wa nyumbani msambaratishie mbali kabisa.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed