2792; Umewafundisha?
Kama watu hawafanyi kitu, kuna sababu mbili tu; HAWAWEZI au HAWATAKI.
Wanakuwa hawawezi pale wanapokuwa hawajui jinsi ya kufanya kitu hicho.
Hilo linakuwa gumu kwao kufanya.
Na mbaya zaidi, watu huwa hawapendi kukiri kwamba hawajui.
Hivyo hujifanya wanajua, lakini kutokujua kwao kunakuwa kikwazo kwenye ufanyaji.
Hapo hujaweka hali ya watu kutokupenda kujifunza.
Unaweza kuona kwa nini ufanyaji wa mambo kwa usahihi inakuwa vigumu.
Wanakuwa hawataki kufanya kitu pale wanapokuwa wavivu na wazembe.
Wanajua kabisa nini wanapaswa kufanya na jinsi ya kukifanya, lakini bado hawafanyi.
Kukosa motisha ndiyo sababu kubwa ya watu kutokutaka kufanya kile wanachopaswa kufanya.
Kama una watu ambao wako chini yako, iwe umewaajiri au wewe ni msimamizi wao, na hawafanyi kile wanachopaswa kufanya, anza kwa kuchukulia hawajui wanachopaswa kufanya.
Hivyo hatua ya kwanza kuchukua ni kuwapa mafunzo sahihi ya kile wanapaswa kufanya.
Mafunzo yahusishe maelezo, mifano na mazoezi.
Hakikisha watu wamejifunza kwa kina, wameelewa na wanaweza kufanya.
Baada ya kuhakikisha umewapa watu mafunzo ya uhakika, angalia kufanya kwao.
Kama bado hawafanyi, basi hapo hawataki tu.
Hatua inayofuata hapo ni kuwapa motisha. Maana tayari wanaweza kufanya, ila wamekosa motisha.
Motisha upo wa aina mbili, chanya na hasi.
Motisha chanya ni pale mtu anapopata zawadi pale anapofanya kitu fulani. Hivyo unaweza kuchagua zawadi gani mtu anapata pale anapofanya. Hilo linawasukuma watu kufanya kwa sababu hakuna asiyependa zawadi.
Motisha hasi ni pale mtu anapopata adhabu anaposhindwa kufanya kitu fulani. Hapa unachagua adhabu ambayo mtu anaipata akishindwa kufanya. Adhabu pia ina nguvu ya kuwasukuma watu kufanya kwa sababu watu hawapendi maumivu au kupoteza.
Kusimamia na kuongoza watu ni jambo lenye changamoto kwa sababu kila mtu ana mtazamo wake tofauti.
Ni vyema ukawa na mfumo rahisi unaoutumia mara zote kwa watu walio chini yako ili pia uwasaidie kuwa bora.
Hatua ya kuchukua;
Kwa watu walio chini yako, pitia ufanisi wao na kwa kila mmoja jua ni nini hajui kufanya na kinamkwamisha kuzalisha matokeo bora.
Andaa mafunzo kwa wote walio chini yako ili kuhakikisha kila mmoja anajua jinsi ya kufanya.
Baada ya mafunzo kama mtu bado hafanyi, basi unapaswa kutoa motisha, chanya au hasi.
Tafakari;
Kuongoza na kusimamia watu ni kugumu, lakini hakukwepeki kama unataka mafanikio makubwa.
Hivyo usilikwepe hilo, badala yake lijengee mkakati sahihi na usimamie katika utekelezaji. Wape watu mafunzo na motisha na wataweza kufanya makubwa zaidi ya wanavyofanya sasa.
Na hilo pia lifanye kwako mwenyewe, pata mafunzo endelevu na kuwa na mfumo wa kukupa motisha wa kuendelea kufanya.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed