2793; Eneo lako la nguvu.
Jamii huwa inapenda kuwadhibiti na kuwatawala watu.
Na ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, hatua kubwa na ya kwanza ambayo jamii huwa inafanya ni kuhakikisha mtu hawi yeye.
Kwa sababu inajua mtu ana nguvu na mamlaka makubwa sana pale anapokuwa yeye, anapokuwa halisi kwake.
Hivyo inakuondoa kwanza kwenye uhalisia wako ili upoteze nguvu na mamlaka yako na uitegemee jamii ambayo itakudhibiti na kukutawala itakavyo.
Kila kiumbe hai kina mahali pake ambapo kina nguvu sana na kikiondoka hapo kinapoteza nguvu zake.
Jaribu kumuua mamba akiwa nchi kavu na unaweza kufanikiwa kirahisi, maana akiwa nchi kavu hana nguvu sana.
Lakini jaribu kumuua mamba huyo huyo akiwa kwenye maji na rafiki yangu utakuwa na kibarua kizito mno.
Mamba anakuwa na nguvu za ajabu anapokuwa ndani ya maji.
Kuna eneo ambalo wewe una nguvu kubwa sana, lakini jamii imekutenga na eneo hilo.
Imekushawishi kwamba siyo eneo muhimu au haliwezi kukupa mafanikio.
Imekuhadaa kwa njia mbalimbali uende kwenye maeneo mengine ambayo kwa nje yanaonekana kuwa na mafanikio, lakini unapoingia ndani unajiona kabisa kwamba huna nguvu.
Ni wakati sasa wa kurejea kwenye eneo lako la nguvu ili uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Uzuri ni kwamba, dunia ya sasa si kama ya zamani.
Zamani uliweza kushawishiwa kwamba kitu fulani hakifai au hakiwezi kukupa mafanikio.
Lakini sasa kuna utandawazi mkubwa ambapo ni rahisi kuona wengine ambao wamefanikiwa sana kwenye kila kitu.
Hivyo ni uhakika kwamba na wewe unaweza kufanikiwa kwenye kile ambacho nguvu zako zipo, kile ambacho una msukumo mkubwa wa kukifanya.
Hatua ya kuchukua;
Ni kitu gani ambacho huwa una msukumo mkubwa wa kukifanya ndani yako lakini jamii imekushawishi kwamba siyo kizuri au sahihi kwako?
Kama bado kitu hicho kinarudi kwako licha ya kukimandamiza, ni ujumbe muhimu kwamba hapo ndipo penye nguvu zako.
Usiendelee kujipunja, badala yake zama kwenye kile kilicho ndani yako kweli na hutaweza kuzuilika.
Tafakari;
Kuna moto ambao huwa hauzimi kabisa pamoja na juhudi zote zinazoweza kutumika kuuzima.
Huenda kuna vitu umekuwa unapenda na kukubali sana tangu ukiwa mtoto.
Lakini jamii ikakuhadaa kwamba siyo vitu sahihi kwako.
Ukaisikiliza jamii, ukafanya ilivyokuambia.
Lakini bado hata sasa vitu vile havijaondoka kabisa ndani yako.
Huko ndiko kwenye nguvu yako kubwa.
Rudi ukaitumie vizuri.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed