2866; Kutokufanya maamuzi thabiti.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye kila ukianzisha jambo linaishia njiani.

Unaweza kujipa sababu nyingi zinazopelekea hilo kutokea.
Na sababu hizo nyingi zitakuwa ni za nje.

Lakini sababu moja kubwa hutaipa uzito, sababu ambayo inaanzia ndani yako mwenyewe.

Sababu hiyo ni kutokufanya maamuzi thabiti.

Neno maamuzi limekuwa linatumika kirahisi sana.
Lakini kiuhalisia maamuzi ni tukio kubwa na lenye nguvu.

Asili ya neno maamuzi ni kukata, kuachana na vitu vingine vyote na kuchagua kimoja.

Maana yake ni kuamua ni kuachana na mengine yote na kuchagua moja ambalo ndiyo muhimu zaidi.

Umakini wako wote unakwenda kwenye lile ulilochagua na siyo kwingine kokote.

Umakini wako ukishagawanyika tu, nguvu yake inapungua na maamuzi unayokuwa umeyafanya yanakosa nguvu.

Tuone mfano kwenye asili ili tuelewane vizuri.
Simba anapoona kundi la swala, anajua pale kuna kitoweo chake.
Lakini hawezi kukimbiza kundi lote la swala.
Hivyo huwa anachagua swala mmoja atakayemkimbiza mpaka kumkamata.
Na mara zote simba huwa wanachagua wanyama wenye wasiwasi na ambao hawajafanya maamuzi thabiti.
Mnyama akishasita sita, simba anajua hapo kuna uhakika wa chakula.

Na kw upande mwingine, simba akishachagua mnyama atakayemkimbiza, atamkimbiza huyo mmoja mpaka amkamate au awe amemkosa kabisa.
Hahangaiki na wanyama wengine bali yule aliyemchagua.

Kila wakati amua kipi kinakuwa kipaumbele namba moja kwako kisha vingine usiruhusu vikaondoa umakini wako kwenye kilicho muhimu zaidi.

A.M.U.A.
Ni hitaji la kwanza na muhimu kwako kupata kila unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.