2867; Asili ya binadamu.
Kwako rafiki yangu ambaye umedhamiria kuwabadili watu.
Nia yako ni njema kabisa, kwa sababu namna watu walivyo inaweza kuwa kikwazo kwao na hata kwako kufanikiwa.
Lakini wajibu huo uliojipa ni mkubwa sana na ambao hauwezekani.
Najua hili litakushangaza, hasa kwa kuwa nimekuwa nakuambia hakuna kisichowezekana.
Lakini ukweli ni kwamba kuwabadili watu ni kitu ambacho hakiwezekani.
Tena kadiri unavyotumia nguvu kubwa kutaka kuwabadili watu, ndivyo nao wanavyotumia nguvu kubwa kuyapinga mabadiliko hayo.
Watu ni wagumu kubadilishwa kwa sababu ya asili ya binadamu.
Kuna vitu watu wanafanya, ambavyo hata wao wenyewe hawajui kwa nini wanafanya.
Ni ile asili ya binadamu iliyo ndani yao ndiyo inafanya baadhi ya mambo bila hata ya mtu kujua.
Kwa mfano, tamaa na hofu. Hivi ni vitu ambavyo vipo ndani ya kila mtu kwa asili kabisa. Kupenda kupata vitu vizuri na kuepuka vitu vibaya ni kitu ambacho kipo ndani ya asili yetu binadamu kabisa.
Watu wapo tayari kuiba, kudanganya, kulaghai na mengine yote ili tu kupata kilicho kizuri na kuepuka kilicho kibaya.
Hivyo basi, badala ya kuweka nguvu zako kubwa kuwabadili watu, jenga mfumo ambao utakuepusha na madhara ya tabia za watu.
Kwa mfano kwa sababu unajua watu wana tamaa ya vitu vizuri na hivyo watashawishika kukuibia pale inapowezekana, ondoa mazingira yanayowawezesha kukuibia.
Ziba kila mianya ya wao kuweza kutekeleza adhma yao.
Hapo utakuwa umelitatua tatizo bila kuhangaika kuwabadili watu.
Kadhalika kwenye kazi, kwa asili watu ni wavivu, wanataka wapate pesa nyingi bila hata ya kufanya kazi kabisa.
Hivyo mfumo unaporuhusu watu kunufaika bila ya kazi, watautumia kujinufaisha.
Badala ya kuhangaika kuwafanya watu wapende kazi, wewe weka mfumo ambao utazuia watu wasinufaike kama hawafanyi kazi.
Huwezi kuwabadili watu, bali unaweza kuzuia madhara ya tabia za watu yasikuathiri wewe. Na hapo ndipo pa kuweka juhudi zako kubwa.
Watu wataendelea kuwa watu, kwa asili yao kama wanadamu.
Wewe una wajibu wa kuhakikisha asili ya binadamu haiwi kikwazo kwako kupata unachotaka.
Na hilo linawezekana kwa nafasi kubwa sana. Ni wewe tu kuweka mifumo sahihi ambayo haitoi mwanya kwa watu kutekeleza asili zao zenye madhara kwako.
Nimalizie tu kwa kukusisitiza wewe rafiki yangu, usihangaike na kuwabadili watu. Bali hangaika kuweka mifumo ambayo tabia na asili ya watu haviwezi kuleta madhara kwako.
Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.