2895; Hakuna asiyefukuzika.
Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye umeshaliona tatizo kwenye biashara yako, lakini unashindwa kulitatua kwa sababu unaona kuna watu hawagusiki.
Unaona ukiwagusa wale ambayo ndiyo chanzo cha matatizo ambayo biashara inayapitia, basi biashara itatikisika sana.
Hilo linakufanya uendelee kukumbatia uvivu na uzembe unaokusumbua sana.
Nina mambo machache ya kuteta na wewe rafiki yangu juu ya hili;
Moja ni hakuna asiyefukuzika kwenye biashara. Wote waliopo kwenye biashara, ukiwepo na wewe mwenyewe, mnafukuzika.
Kwa mfano ikitokea biashara imekufa, moja kwa moja wote mnakuwa mmefukuzwa.
Mbili ni siyo wewe unayepaswa kuwaondoa watu kwenye biashara, bali mfumo wa biashara unaokuwepo ndiyo unaowaondoa watu.
Watu wanaukimbia mfumo kwa kuona ni mgumu au mfumo unawaengua wale ambao hawawezi kuenda nao.
Tatu ni mwenye maumivu kwenye biashara ni wewe. Ikitokea leo biashara imekufa ni wewe mmiliki ndiye unayepata hasara yote.
Wafanyakazi wako, hakuna anayeingia hasara unayoingia wewe.
Jikumbushe hili kila mara ili uweze kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya biashara yako.
Nne ni matatizo mengi huwa yanaanzishwa na/au kuchochewa na mtu mmoja au wachache. Ukiwatambua hao na kuwaondoa, utakuwa umeisaidia sana biashara yako.
Tano ni kama biashara yako itayumba sana kwa kumwondoa mfanyakazi ambaye ni changamoto, basi jua una tatizo kubwa zaidi. Maana kitendo cha kuwaacha wale ambao ni mzigo, kitaiua biashara yako mapema sana. Ni bora uchukue hatua mara moja kama ni kufa ife mapema na uwe umejifunza.
Rafiki yangu mpendwa, naamini umeelewa hili kwa kina. Lifanyie kazi kwa uhakika ili uweze kujenga biashara ambayo itadumu vizazi na vizazi.
Weka mfumo wa kuiendesha biashara ambao utawatema wale wasio na sifa sahihi.
Mwisho kabisa, kila mara jikumbushe kwamba kila mtu anafukuzika kwenye biashara, ikiwepo wewe mwenyewe. Hilo litafanya vitu viweze kuonekana kwa mtazamo sahihi.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe