2897; Sababu hazitauza.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayeshangaa kwa nini unashindwa kuuza licha ya juhudi kubwa unazoweka.
Kinachokuzuia kuuza ni sababu nyingi unazokuwa nazo juu ya yale unayofanya au kushindwa kufanya.
Unashindwa kukaa kwenye mchakato na kutekeleza viwango ulivyojiwekea. Badala ya kukubali uvivu na uzembe uliopelekea hayo, wewe unajipa sababu na visingizio.
Kadiri unavyokuwa mwepesi kutoa sababu, ndivyo pia unavyokuwa ngumu kutoa matokeo.
Sababu na matokeo ni vitu ambavyo haviwezi kulala kwenye kitanda kimoja.
Tunachotaka ni kuachana na sababu na kuzalisha matokeo.
Mauzo ni mchezo ambao uko wazi kabisa kwenye kupima matokeo. Ni umeshinda kwa kuuza au umeshindwa kwa kutokuuza.
Unaweza kujipa sababu nyingi uwezavyo za kushindwa kuuza, lakini hakuna sababu hata moja itakayobadili kushindwa kuwa ushindi.
Ushindi hautaletwa na maelezo ya sababu, hata yawe mazuri kiasi gani.
Ushindi utaletwa na kukaa kwenye mchakato sahihi wa mauzo bila kuyumbishwa na chochote.
Usipende sana kuwa mtu wa kutoa sababu. Badala yake kuwa mtu wa kuonyesha mchakato na matokeo unayopata.
Kama umeshindwa kukaa kwenye mchakato wako na kuonyesha matokeo, wala usipoteze muda wako kueleza sababu zilizopelekea ushindwe. Unapaswa kukaa kwenye mchakato na kuonyesha matokeo na siyo sababu.
Unajua wajibu wangu mkuu kwako wewe ambao ni kuhakikisha unajenga na kukuza biashara kupitia kuwa na timu imara na kukuza mauzo.
Hayo yatawezekana kwa kukaa kwenye mchakato na kuonyesha matokeo, siyo kwa kutoa sababu lukuki.
Unaweza kuwa na sababu nzuri sana kwa upande wako, lakini ninachoomba ni usizilete kwangu. Badala yake niletee mchakato na matokeo. Nionyeshe nini umefanya na matokeo uliyopata ni yapi. Hili linakupa matokeo mazuri kuliko sababu.
Nipe mchakato na unipe matokeo, sitaki unipe sababu.
Maana haijalishi una sababu nzuri kiasi gani, hazitauza.
Ujue mchakato wako kamili kwenye mauzo na hakikisha unaufuata huo mara zote bila kuacha. Hilo lina nguvu kubwa ya kuongeza sana matokeo yanayohitajika.
Kila unapojikuta ukijiandaa kutoa sababu iliyokukwamisha usiuze, jikamate kwa kuyaacha hayo maelezo ya sababu na kukaa kwenye mchakato. Mchakato utakupa matokeo mazuri kuliko sababu.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe