3135; Utamchagua nani?

Rafiki yangu mpendwa,
Safari yetu ya mafanikio makubwa tunayoyataka inawategemea sana watu.
Hakuna namna tunaweza kufikia mafanikio makubwa kabisa sisi peke yetu.

Kadiri lengo letu la mafanikio linavyokuwa kubwa, ndivyo pia idadi ya watu tunaowahitaji inavyokuwa kubwa zaidi.
Hivyo sehemu kubwa sana ya maamuzi utakayokuwa unayafanya kila siku ni kuhusu NANI (WHO) na siyo NINI (WHAT) au VIPI (HOW).

Ili kulitafakari hilo vizuri, fikiria mifano hii mitatu;

Moja; fikiria umeambiwa hutaruhusiwa tena kufanya kazi kwa maisha yako yote. Unatakiwa umchague rafiki yako mmoja ambaye utapata asilimia 10 ya kipato chake kwa kipindi chote cha maisha yako kilichobakia.

Je utamchagua rafiki yupi ambaye una uhakika kwamba kwa mwenendo wake utaweza kufikia malengo uliyonayo?

Nini kimekufanya umchague rafiki huyo?

Kama kwa marafiki ulionao sasa huoni ambaye upo tayari kumchagua, ni mtu mwenye sifa zipi ambaye utakuwa tayari kumchagua kwenye zoezi hilo?

Majibu uliyojibu hapo, ndizo tabia ambazo wewe mwenyewe unapaswa kuwa nazo.
Kwa sababu kwa kuwa na tabia hizo, utawavutia wale wenye tabia za aina hiyo na mtaweza kuambatana kwenye safari ya mafanikio makubwa kwenye maisha.

Mbili; fikiria wateja wote ulionao kwenye biashara yako wanaondolewa na unaachiwa mteja mmoja tu.
Mteja huyo mmoja ndiyo wateja wengine wote wa biashara yako watatokea kwake.

Je utamchagua mteja yupi ambaye una uhakika kwamba kupitia yeye utaweza kupata wateja wengine bora?

Nini kimekufanya umchague mteja huyo?

Kama kwa wateja ulionao sasa huoni ambaye upo tayari kumchagua, ni mteja mwenye sifa zipi ambaye utakuwa tayari kumchagua kwenye zoezi hilo?

Utamtunzaje huyo mteja ili uweze kupata wengine wengi kupitia yeye?

Majibu uliyojibu hapo, ndizo tabia ambazo unapaswa kuziangalia kwa wateja na jinsi unavyopaswa kwenda nao.

Tatu; fikiria wafanyakazi wote ulionao kwenye biashara yako wanaondolewa na unaachiwa mfanyakazi mmoja tu.
Wafanyakazi wengine wote unaowahitaji watatoka kwa mfanyakazi huyo mmoja.

Je utamchagua mfanyakazi yupi ambaye una uhakika kwamba kupitia yeye utaweza kupata wafanyakazi wengine bora?

Nini kimekufanya umchague mfanyakazi huyo?

Kama kwa wafanyakazi ulionao sasa huoni ambaye upo tayari kumchagua, ni mfanyakazi mwenye sifa zipi ambaye utakuwa tayari kumchagua kwenye zoezi hilo?

Utamtunzaje huyo mfanyakazi ili uweze kupata wengine wengi kupitia yeye?

Majibu uliyojibu hapo, ndizo tabia ambazo unapaswa kuziangalia kwa wafanyakazi na jinsi unavyopaswa kwenda nao.

Rafiki, naamini zoezi hilo limekupa mwanga wa tofauti kabisa juu ya watu wa kushirikiana na kuambatana nao kwenye maisha yako ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Tumia zoezi hili kama msingi wako mkuu wa kuchagua watu sahihi na kujua jinsi ya kwenda nao ili uweze kupata matokeo unayoyataka.

Watu ndiyo watakaojenga au kuvunja mafanikio yako.
Lakini bado huwezi kuwalaumu watu kwa chochote kwenye maisha yako, kwa sababu ni wewe ndiye unayewachagua, iwe unajua au hujui.
Wajibu wako mkubwa ni kuwachagua watu sahihi ambao unajua kwa mwenendo wao watajenga mafanikio yako na siyo kuyabomoa.

Weka juhudi kubwa kwenye kupata na kujenga watu sahihi, huku ukijua huwezi kuwabadili watu, ndiyo maana unatakiwa kuanza na wale ambao tayari ni sahihi.

Maamuzi ya NANI yatakuwa endelevu kwa maisha yako yote.
Kuna ambao utawashusha kwenye basi, yaani kuachana nao kwa sababu umeona hawajengi bali kubomoa na kuna ambao utawapakiza kwa sababu kuna vitu umeona kwao.

Zoezi la kushusha na kupandisha watu litakuwa endelevu kwenye maisha yako.
Usilichukulie kama kushindwa.
Ni sehemu ya kawaida kabisa kwenye safari yako ya mafanikio, kwa sababu mpaka uwapate watu sahihi kabisa huwa inachukua muda.

Kitu muhimu kujua wakati wote ni watu sahihi wapo, ni vile tu unakuwa hujaamua ni watu wa aina gani unaowataka na kuweka kazi na muda katika kuwafikia na kuwashawishi kwenda nao.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe