💯KCM2324014; Binafsi
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Binafsi.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo tunapaswa kuitumia siku hii kwa mambo yetu binafsi.
Kwenye siku za wiki ambazo ni za kazi, watu wengi wanakuwa wanataka na kutegemea mengi kutoka kwetu.
Na kwa sababu muda ni mchache na mambo ya kufanya ni mengi, tunajikuta tukihangaika na matakwa ya wengine na kuahirisha ya kwetu.
Katika kukamilisha majukumu yetu mbalimbali ya kikazi na kibiashara, mambo yetu binafsi yanakwama.
Siku ya jumapili, ambayo imezoeleka kuwa ya mapumziko kwa walio wengi, ni nzuri kuitumia kukamilisha mambo yako binafsi yakiyokwama kwa wiki nzima.
Ndiyo maana tumeitenga siku hii kuwa ya mapumziko.
Siyo mapumziko ya kulala siku nzima au kufanya kila aina ya starehe.
Bali ni mapumziko ya kuwazuia wengine wasikusumbue na upate muda kwa ajili yako binafsi.
Kama utawaruhusu watu wakuhangaishe kwa matakwa yao muda wote wa siku na siku zote za wiki, unaweza kujenga kazi au biashara nzuri, lakini ukayapoteza maisha yako.
Unapumzika jumapili kwa upande wa kazi na biashara, lakini unafanyia kazi mambo yako binafsi.
Unaangalia yale mambo yako muhimu yaliyokwama kwenye wiki kwa sababu ulikosa muda kwa kutingwa.
Kisha unahakikisha umeyakamilisha kwenye kila jumapili.
Jumapili unapumzika kuhangaishwa na wengine, lakini unajihangaisha mwenyewe.
Hili ni hitaji muhimu sana la kujenga maisha bora kwako.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu sifa za watu wa kushirikiana nao. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/12/3238
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku unayokwenda kukamilisha mambo yako binafsi yaliyokwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako kuu.
Kocha.
💯